Mfanyabiashara azimwa kuvamia shamba la bwanyenye marehemu
NA RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA Kuu imemzima mfanyabiashara Dorcus Joan Kiptoo kutwaa umiliki wa shamba la ekari 66 lenye thamani ya Sh4.6 bilioni la mtu aliyeaga dunia.
Jaji Oguttu Mboya alitoa maagizo hayo baada ya kufahamishwa na msimamizi wa mali ya marehemu Kanji Naran Patel kwamba wahuni walioandamana na Bi Kiptoo walivamia shamba hilo lililoko mtaani Karen mnamo Machi 2, 2024, na kusababisha uharibifu mkubwa.
Jaji Mboya aliwaamuru Naibu Kamanda wa Polisi Kaunti ndogo ya Karen/Langata pamoja na OCS Kituo cha Polisi cha Karen wahakikishe Bi Kiptoo na washtakiwa wengine wawili hawajaingia katika shamba lile.
Jaji Mboya aliwataka maafisa hao wakuu wa polisi wahakikishe amani inadumishwa na hakuna visa vya utovu wa nidhamu vitakavyotokea.
Jaji Mboya aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kumwamuru Bi Kiptoo ajibu madai kwamba alivamia shamba la wenyewe mtaani Karen kinyume cha sheria.
Jaji huyo alisema kesi ya Patel iko na mashiko kisheria na kutoa maagizo ya muda ya kuwazima washtakiwa kuvamia shamba hilo.
“Hii mahakama imeridhika kwamba kesi ya Patel iko na mashiko kisheria na kwamba Bi Kiptoo na maajenti wake au wafanyakazi wake wamezuiwa kuingia au kuvuruga umiliki wa shamba hilo hadi kesi hii isikilizwe na kuamuliwa,” Jaji Mboya aliamuru.
Katika kesi hiyo Bw Arvind Kanji Patel, mwanawe marehemu Naran, alisema endapo mahakama haitaingilia kati, bila shaka shamba hilo litanyakuliwa na wavamizi kinyume cha sheria.
Arvind aliwasilisha kesi hiyo chini ya sheria za dharura na kuomba mahakama itumie uwezo wake kuokoa shamba lao.
Arvind alimweleza Jaji Mboya kwamba uvamizi huo ulipofanywa, maafisa wa polisi wa utawala walikuwa pale na walitazama tu mijengo ikibomolewa na mapaa ya nyumba yaking’olewa bila kufanya chochote kuzuia uhalifu.
Arvind alimsihi Jaji Mboya azime hatua hiyo ya shamba lao kuvamiwa na watu ambao hawana hatimiliki ama “maagizo kutoka mahakamani waingie shambani mwake.”
Mlalamishi huyo amewashtaki Bi Kiptoo, Msajili Mkuu wa Ardhi, Mkurugenzi wa Usoroveya na Mwanasheria Mkuu.
Arvind anaomba mahakama itumie uwezo wake kuokoa na kutetea mali ya baba yao wanayoirithi lakini inayonyemelewa na mabwanyenye.