• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 AM
Migodi ya dhahabu ilivyogeuka kuwa ngome ya mauti 

Migodi ya dhahabu ilivyogeuka kuwa ngome ya mauti 

NA OSCAR KAKAI

ENEO la Romus katika Lokesheni ya Lopet, wadi ya Kiwawa mpakani mwa Kaunti ya Pokot Magharibi na Turkana ni limesheheni mazingira ya miba, vumbi na misitu.

Romus, ina utajiri na shughuli nyingi za kuvutia sio tu kwa wakazi bali pia kwa wageni ambao hufika kusaka dhahabu.

Eneo hilo lina wachuma dhahabu ambao wanasaka maelfu na mamiloni ya fedha.

Kukiwa na wengi wanaojitafutia riziki bila masharti ya serikali, Romus imegeuka kuwa mithili ya Sodom na Gomorrah kutokana na uhuni na mauaji ya mara kwa mara.

Wakazi na wafanyikazi wanaishi kwa hofu, kufuatia mashambulizi yasiyoisha.

Hussein Ibrahim ambaye alisafiri kutoka Mandera kufanya kazi ya kusaka dhahabu anasema anaishi kwa wasi wasi mkuu.

“Tunaishi kwa neema ya Mungu,” Hussein anasema.

Kuongezea chumvi kwenye kidonda kinachouguza, eneo hilo lina uhaba wa maji ikizingatiwa kuwa uvunaji dhahabu ni shughuli inayohitaji raslimali hiyo kwa wingi.

Haron Nyongesa, mfanyakazi mwingine kutoka Bungoma anahoji eneo hilo halikaliki.

“Tunasaka riziki licha ya milio ya kila siku ya risasi zinazofyatuliwa na majangili,” anasema.

Mashambulio ya wizi wa mifugo yanamtia kiwewe kifungua mimba huyu anayetegemewa na familia yake.

Mfanyakazi mwingine, Robert Magesa anasema kuwa anajaribu kujikakamua licha ya visa vya utovu wa usalama japo anahisi mambo sasa yamevuka mipaka.

Uvamizi unaofanyika umepunguza saa za kazi, licha ya maafisa wa usalama kutumwa kushika doria.

“Sisi hufanya kazi saa mbili au tatu pekee kwa sababu ya hofu ya mashambulizi. Barabara za hapa hazipitiki,” anasema Magesa, ambaye ametoka Migori.

Chini ya kipindi cha muda wa mwaka mmoja, zaidi ya watu 10 wamepoteza maisha kwa kuvamiwa wakisaka dhahabu.

Miundomsingi kama vile barabara eneo la Rumus ni duni, bila kusahau mawimbi ya mawasiliano ambayo yanahitaji kuboreshwa.

Shambulizi linapotokea, huchukua maafisa wa kukabiliana na ghasia (GSU) muda mrefu kufika.

Kambi yao iko mbali, hivyo basi kuzidisha maji kwenye unga.

Kutua eneo hilo, utalazimika kutumia barabara ndefu ya Kasei-Romus, yenye misitu ambapo majangili hujificha.

Nayo ruti ya Kapenguria, msafiri analazimika kuenda Turkwel – umbali wa kilomita 250.

Chifu wa Lokesheni ya Lopet, Isaac Lomwai anasema kuwa eneo hilo linahitaji askari wengi wa akiba (NPR) kusaidia maafisa wa polisi kuimarisha usalama.

“Tuna askari wa akiba 14 kati ya 21 kwenye lokesheni, ambao hushika doria eneo la migodi,” anasema.

Kituo cha polisi kilicho karibu kulingana na Chifu Lomwai, ni cha Kasei na kingine eneo la Nakwomoru, Turkana, umbali wa kilomita 100.

Naibu Kamishna Kaunti Ndogo ya Pokot Kaskazini, James Ajuang anasema kuwa kuna mipango ya kujenga kambi ya polisi eneo hilo.

Nayo serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi inasema imeanzisha harakati za kufungua barabara ili kukabiliana wahuni.

  • Tags

You can share this post!

KPC yapiga jeki uhifadhi wa misitu Mombasa

Wanawake wanavyojituma kuzimbua riziki kwenye matimbo...

T L