Habari za Kaunti

Miradi Lamu yaachia wenyeji kicheko na kilio kwa wakati mmoja

May 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

INAAMINIKA kwamba mara nyingi miradi ya maendeleo inapofika au kuanzishwa mahali, basi eneo hilo huishia kukua na kupanuka.

Yaani kubuniwa kwa miradi mahali ni sawa na msemo wa ‘Mgeni Njoo Mwenyeji Apone’.

Na ndio sababu pindi mradi unapotua mahali, utapata miundomsingi muhimu kama vile barabara ambayo awali haikuwapo, ikianza kujengwa.

Pia utapata vituo vya polisi na miradi mingine tanzu ikianzishwa ilmradi kuufanikisha ustawi wa mradi mkuu ulioanzishwa.

Miradi yote kwa jumla huishia kuisaidia au kuibadilishia maisha jamii na kizazi yamkini hata kile kijacho.

Katika kaunti ya Lamu aidha, miradi mingi, hasa ile inayotekelezwa na serikali ya kitaifa imewaachia wenyeji kicheko na kilio kwa wakati mmoja.

Hapa, utapata kwamba mbali na miradi husika awali kuonekana kuwa ya baraka tele kwa jamii, mwishowe miradi hiyo hiyo iligeuka kuwa laana kwao, wengi wakiachwa na dhiki, kilio, majonzi na jakamoyo.

Ikumbukwe kuwa Lamu ni miongoni mwa kaunti ambazo zimebahatika kwa kuwa na miradi mikuu iliyotekelezwa na serikali ya kitaifa.

Miradi hiyo ni pamoja na ule wa Sh310 bilioni wa Bandari ya Lamu ambao ulijengwa, kukamilika na kufunguliwa rasmi na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo Mei 20, 2021.

Mradi huo unapatikana eneo la Kililana, Lamu Magharibi.

Ni mradi ambao tangu uanze umebadili vilivyo maisha ya wakazi wa Lamu na pia kupanua eneo zima la Kaskazini mwa Kenya kibiashara na maendeleo.

Ni mradi ambao umeajiri maelfu ya vijana wa Lamu na kaunti zingine za Kenya.

Kutua kwa mradi huo pia kuliichochea serikali kuu kuanzisha kwa mara ya kwanza katika historia, ujenzi wa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen hadi kutiwa lami kwake.

Barabara hiyo ya kilomita 135 ilijengwa kwa kima cha Sh10.8 bilioni, hivyo kufunguliwa siku hiyo hiyo moja ambapo bandari ya Lamu ilifunguliwa rasmi kuanza shughuli zake za uchukuzi wa meli.

Ujenzi wa bandari ya Lamu na barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen pia umekuwa wa tija tele kwani biashara zimeanzishwa kandokando ya bandari na pembezoni mwa barabara, hivyo kuletea wenyeji na wakazi wa Lamu ufanisi hata zaidi.

Miji inayopakana na mradi wa bandari ya Lamu huko Kililana na ile iliyoko pembezoni mwa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen pia imeshuhudia kukua kwa kiwango kikubwa miaka ya hivi karibuni.

Miji hiyo ni pamoja na Kililana, Mashunduani, Mokowe, Hindi, Magogoni, Kibaoni, Majembeni na viunga vyake.

Sekta za nyumba za kukodi pia zimekuwa zikifaidi kuwepo kwa miradi ya bandari na barabara wakazi wakitumia mwanya huo kujijengea nyumba za kukodi, hoteli na mikahawa, biashara ambazo leo zinazidi kunoga.

Isitoshe, ujio wa Bandari na barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen ulibadilisha maisha ya maskini na kuwa ya tajiri kwani serikali ilijikakamua kuwafidia baadhi ya wale ambao ardhi zao zilitwaliwa kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo.

Barabara ya Lamu-Witu-Garsen. PICHA | KALUME KAZUNGU

Lakini je, kwa nini miradi mikubwamikubwa kama hii yenye kuleta raha mwishowe ikaishia kuwa karaha kwa wakazi.

Baadhi ya waliohojiwa na Taifa Leo walisema katu hawapingi kwamba miradi iliyoanzishwa ni yenye faida kubwa.

Wakazi hao aidha wanashikilia kuwa mbali na uzuri au utamu uliopo wa miradi hiyo, pia hawawezi kusahau upande mwingine ambapo kwa wengine, wanahisi uchungu.

Bw Mohamed Rajab, mkazi wa Lamu anasema hawezi kusahau jinsi serikali ilivyowanyanyasa ardhi zao zilizotwaliwa kwa ujenzi wa Bandari ya Lamu eneo la Kililana bila ya kuzingatia kuwafidia kikamilifu.

Bw Rajab, ambaye ni msemaji wa Muungano wa Wakulima wa Kililana, kila kuchao amekuwa akiililia serikali na Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC) kuhakikisha haki imetendeka kwao.

Bandari ya Lamu na miradi tanzu yake ilitengewa ardhi ya ekari 70,000 kwenye eneo la Kililana na Mashunduani.

Mnamo Februari 2015, serikali ya kitaifa kupitia NLC ilitoa Sh1.3 bilioni kuwafidia zaidi ya waathiriwa 140 wa ardhi za bandari ya Lamu.

Bw Rajab aidha anashikilia kuwa Sh1.3 bilioni zilizotolewa kufidia waathiriwa hazitoshi, ikizingatiwa kuwa ardhi iliyotwaliwa ni kubwa.

“Wao walitupiga chenga. Ekari za ardhi walizofidia ni kidogo ilhali ardhi waliyochukua ni kubwa mno. Tuko na karibu ekari Zaidi ya 5000 za ardhi yetu ambayo sisi hatukulipwa. Kila tukiuliza tunapelekwa visivyo. Tunaomba serikali isikie kilio chetu. Tunateseka na familia zetu. Twahitaji fidia pia,” akasema Bw Rajab.

Naye Mwanamina Amin, mkazi wa Mashunduani, anasema hatua ya ardhi zao kujumuishwa kisiri kwa zile zilizofidiwa kwa minajili ya ujenzi wa bandari ya Lamu ni dhihirisho tosha kwamba wahusika walitaka kuwanyanyasa kwa kuwanyima haki yao ya fidia.

Bi Amin alisema licha ya bandari ya Lamu kuwa mradi wa manufaa tele, upande wao wanaishi kiskwota.

“Mradi ulituletea kisirani. Tulitolewa kwenye ardhi zetu za kijamii bila ya kufidiwa. Twadai haki yetu,” akasema Bi Amin.

Kuwepo kwa miradi ya bandari ya Lamu na barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen pia kumesukuma dhuluma, hasa unyakuzi wa ardhi kuendelezwa.

Mabepari wengi wamekuwa wakijihami kwa hatimiliki feki za ardhi, ambapo wamekuwa wakitumia uwezo wao mkubwa wa kifedha kuwafurusha wananchi maskini kutoka kwa mashamba yao.

“Miradi ya serikali, hasa Bandari ya Lamu, imechangia maovu kuendelezwa eneo hili. Kuna watu wanaodhulumu wengine ardhi zao kwa kutumia uwezo wao wa kifedha. Haya yote yanatokana na hadhi ambayo ardhi zinazokaribiana na bandari ya Lamu ziko nayo. Maskwota wameongezeka Lamu kutokana na dhuluma hizi,” akasema Ahmed Yusuf, mkazi wa Mokowe.