Habari za Kaunti

Miradi mikuu kuua ladha ya feri Likoni

January 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WINNIE ATIENO

FERI tano kwenye kivuko cha Likoni kinachounganisha Kisiwa cha Mombasa na Mombasa Kusini huenda zitaacha kutumiwa hivi karibuni, huku miradi miwili mikuu ya miundomsingi ikiendelea kukamilishwa.

Huku barabara kuu ya Dongo Kundu inayounganisha Mombasa na Kaunti ya Kwale ikikaribia kufunguliwa kwa matumizi ya umma, mradi wa Daraja la Mombasa Gate linalounganisha Mombasa Kusini na Kisiwa cha Mombasa eneo la Likoni pia umepigwa jeki baada ya muda mrefu.

Ujenzi wa daraja la Mombasa Gate kwa kima cha Sh47 bilioni unatarajiwa kuanza kwani Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) na Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu za Kenya (KeNHA) zimekamilisha mipango yao.

Daraja hilo la kilomita 1.4 linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36. Kenya na Japan zilitia saini mkataba wa mkopo wiki jana kwa ajili ya ufadhili huo.

Wizara ya Uchukuzi na Barabara imesema mkataba wa mkopo unafungua njia ya kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo mara moja.

Awali mradi huo ulipangwa kuanza Juni 2021 na kukamilika mwaka huu lakini ulichelewa kutokana na changamoto za fidia na kusababisha kuahirishwa.

Kulingana na mipango ya ujenzi, daraja litakuwa na njia nne za trafiki na litakuwa na urefu wa mita 69 katikati, na hivyo kuacha nafasi ya kutosha kwa meli kuvuka chini yake.

Kwa sasa, kituo cha feri cha Likoni husafirisha takriban abiria 300,000 na zaidi ya magari 6,000 kila siku.

Feri hizo pia zimekuwa zikitumika kama kivutio cha utalii mjini Mombasa. Hata hivyo, hitilafu za mara kwa mara na msongamano umekuwa jinamizi kwa watumiaji wa feri, hasa kwa sekta ya utalii.

Wadau katika sekta ya hoteli walisema miradi hiyo itaimarisha utalii na kulifanya eneo la Pwani kuwa kitovu cha uwekezaji ambacho kitavutia wawekezaji wa kimataifa.

“Tunafurahishwa na maendeleo ya miundombinu zinazoendelea katika eneo la Pwani kwa sababu zinaendana na maendeleo ya utalii, hasa baada ya kukamilika kwa barabara ya Dongo Kundu, na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Diani. Inatoa mtazamo wa jumla wa mji wa kitalii,” alisema Afisa Mtendaji wa Chama cha Wahudumu wa Hoteli na Wahudumu (KAHC), Dkt Sam Ikwaye.

Kulingana na maelezo kuhusu daraja hilo, Shirika la Huduma za Feri nchini linatarajia kupoteza mapato mara tu daraja hilo litakapoanza kufanya kazi.

Hata hivyo, wadau wa shirika hilo walisema linaweza kuhamia maeneo mengine kutokana na majukumu yake ya kitaifa.

Kuhusu uhamishaji wa watu, tafiti zilibainisha Majengo, Likoni, Mtongwe, Shika Adabu na Ngombeni kuwa miongoni mwa maeneo yatakayoathirika zaidi na ujenzi huo.

Zaidi ya nyumba 1,200 na majengo yenye thamani ya mamilioni ni miongoni mwa vinavyotarajiwa kuathirika vilevile.

Baadhi ya mali za tangu jadi zitakazohamishwa ni pamoja na Baa ya Kilindini ambayo ilianzishwa mwaka 1908, na kuwa baa kongwe zaidi eneo la Pwani.

Katika mkutano huo uliofanyika wiki jana, Waziri wa Uchukuzi na Barabara Kipchumba Murkomen alisema daraja hilo litatoa manufaa zaidi ya kiuchumi kwa ukanda wa Pwani na Kenya kwa ujumla.

“Haitarahisisha tu usafirishaji wa watu na bidhaa kati ya Kisiwa na Pwani ya Kusini lakini pia itakuwa kivutio cha watalii,” akasema.

Kwa upande wake, Katibu wa Barabara Joseph Mbugua, alisema mradi huo utaajiri karibu Wakenya 80,000 wakati wa ujenzi na kuzalisha mapato ya karibu Sh80 milioni kwa mwaka.