Miradi yangu si ukora wala danganya toto, asema Ruto
RAIS William Ruto amewataka Wakenya waamini miradi yake ya kuwapiga jeki kiuchumi, akisema mipango yake si ukora jinsi ambavyo baadhi ya wapinzani wake wanavyodai.
Kiongozi wa nchi aliwataka Wakenya wasisikilize propaganda au wanaozungumzia kile ambacho hawakielewi, akisema nia yao ni kuwazuia watu kunufaika kwa miradi ya serikali.
“Msikubali propaganda kutoka kwa watu wasiokuwa na mwao kuhusu yanayofanyika. Wengi watakuambia mpango wa NYOTA ni ukora,” akasema Rais.
“Hiyo inamaanisha vijana ambao wako hapa ni wakora? Ninyi ni mashujaa kwa sababu mlikubali kuja hapa kupokea hela za mpango wa Nyota,” akaongeza.
Aliongea hayo katika uwanja wa Gusii alipoongoza hafla ya kusambaza pesa kwa vijana chini ya mpango huo. Vijana waliolengwa walitoka kaunti za Kisii, Nyamira na Migori.
“Msiwaamini wapinzani hao kwa sababu hawana chochote cha kutupatia. Hawana mpango, hawana ajenda, hawana ruwaza na hawawezi kutuambia chochote,” akasema huku akisisitiza ataendelea kushiriki mipango hiyo ya kuwainua Wakenya kimapato.
Zaidi ya vijana 8,820 kutoka kaunti hizo watanufaika kwa Sh220.5 milioni baada ya kupata mafunzo ya lazima ya siku nne.
Mafunzo hayo yatawapa ujuzi wa kutumia pesa hizo kwa biashara au miradi itakayowaongezea mapato ili wajizimbulie riziki.
Rais pia alitumia hafla hiyo kurai jamii ya Gusii imuunge mkono huku akianika miradi ambayo utawala wake unapanga kutekeleza kwa eneo hilo.
Wakati wa ziara hiyo, alipokelewa na Gavana wa Kisii Simba Arati pamoja na mwenzake wa Nyamira Amos Nyaribo ambapo Rais alisisitiza kuwa yupo tayari kushirikiana nao kuendeleza eneo hilo kiuchumi.
Pia rais alikuwa ameandamana na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, Kiongozi wa wachache na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, Kiranja wa Wengi Sylvanus Osoro, Waziri wa Elimu Julius Ogamba na wabunge na madiwani kutoka kaunti za Kisii na Nyamira.
Ni wakati wa hafla hiyo alitangaza kuwa gereza la Kisii litahamishwa kutoka mjini na kujengwa nje ya mji huo.
Mabw Arati na Nyaribo walisifu mradi wa Nyota akisema utasaidia vijana kujiajiri na kujisimamia kimapato.
Bw Nyaribo aliwataka waliopewa pesa hizo wazitumie vizuri akisema kaunti yake haitawatoza hela za leseni za kufanya biashara.