Mkibebwa mbebeke, Chibule ashauri wakazi wa Kilifi
NA JURGEN NAMBEKA
NAIBU Gavana wa Kilifi Florah Chibule amewataka wakazi wa Pwani wanaofaidika na miradi ya kiufadhili kutoka nchi za ng’ambo, kutumia vyema nafasi hiyo kama njia ya kuhakikisha jamii inafaidika kwa muda mrefu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuchakata muhogo katika eneo la Chumani, Kaunti ya Kilifi, Bi Chibule alieleza kuwa kwa kutumia miradi hiyo vyema, washikadau wanapata hamu ya kuongeza miradi mingine.
“Leo tumekabidhiwa mradi na wafadhili wa Umoja wa Bara Ulaya chini ya mradi wa Go Blue. Ninachoomba ni kuwa tuendelee kutafuta mbinu zaidi za kuhakikisha tunatumia mtambo huu vizuri. Kwa kuhakikisha unatumika vyema serikali ya kaunti itawazia kuwekeza katika mradi wa ziada katika mchakato mzima,” akasema Bi Chibule.
Kulingana naye, tayari wafadhili hao walikuwa wameshawapa wakazi njia ya kuongeza thamani muhogo na kuwawezesha kuuza.
“Tumeona kuwa hapa muhogo unaweza kutolewa magamba, ukavunjwa vunjwa, kukaushwa na kusagwa unga. Tumesikia kuwa mumeeleza munahitaji sehemu ya kuoka bidhaa na hilo litatekelezwa kwa kuona juhudi zenyu,” akasema Bi Chibule.
Mwakilishi Wadi ya Matsangoni Bw Hassan Mohamed, alionya kuwa mara nyingi miradi inapoanza na vikundi vidogo huwa inafanya vizuri ila huharibika pale ambapo pesa huanza kuingia.