Habari za Kaunti

Mombasa kuchanja madereva wa malori dhidi ya Mpox msambao ukizidi

Na WINNIE ATIENO August 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI ya Mombasa imepokea dozi 5,000 za chanjo za kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Mpox, unaoendelea kusambaa kwa kasi katika jiji hilo.

Kaunti ya Mombasa imebainishwa kuongoza kwa idadi kubwa ya maambukizi ya homa hiyo nchini.

Hata hivyo, ili kukabiliana na ugonjwa huo, Serikali Kuu imeanza kupeana chanjo kwa kaunti zilizoathirika zaidi hasa Mombasa.

“Tumepokea chanjo 5,000 za mpox na tunalenga kuwapatia wale ambao wako kwenye hatari ya kuambukizwa ambao ni ni pamoja na madereva wa malori kuanzia mwezi wa Septemba,” alisema mshirikishi mkuu wa chanjo Kaunti ya Mombasa, Bw Imani Baraka.

Bw Baraka alisema maeneo ya Jomvu na Changamwe ndiyo yaliyoathirika zaidi katika Kaunti ya Mombasa.

Wizara ya Afya imetangaza kuwa nchini kuna visa 420 vya mpox katika kaunti 26 tangu mlipuko wa homa hiyo ulipotangazwa Julai mwaka jana katika kaunti ya Taita Taveta.

Kisa hicho kilihusisha dereva wa lori ambaye alikuwa amesafiri kutoka nchi jirani ya Uganda.

Kufikia sasa watu sita wameaga dunia huku wagonjwa 39 wakilazwa kutokana na ugonjwa huo.

Kulingana na takwimu kutoka kwa wizara hiyo, wagonjwa wengine 80 wanaendelea kuuguza ugonjwa huo nyumbani huku wengine 295 wakiripotiwa kupona.

Kaunti ya Meru iliripoti kisa cha kwanza cha homa ya nyani hapo jana.

Wizara ya afya iliwataka wakazi kuchukua tahadhari kufuatia ongezeko la visa vya ugonjwa huo hatari.

Mpox ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi na huambukizwa kwa njia ya kugusana kwa karibu na mtu aliyeambukizwa au vifaa alivyotumia kama vile nguo na shuka.

Dalili zake ni pamoja na homa kali, maumivu ya misuli, kuvimba mwilini na upele unaoenea sehemu mbalimbali za mwili hata sehemu za siri. Baadhi ya visa vimehusishwa na wasafiri kutoka Uganda na Rwanda, ambako Mpox pia imeripotiwa kwa wingi.

“Kaunti ya Mombasa inaongoza kwa maambukizi, kwa sasa ikinakili visa 178,” ripoti ya Wizara ya Afya ilisema.

Wasafiri milioni 6.2 wanaoingia humu nchini kupitia mipakani kutoka nchi ambazo zimeripoti ugonjwa huo pia wamepimwa.

Kaunti zilizoathirika ni pamoja na Busia (65), Nairobi (45), Makueni (25), Nakuru (22), Kilifi (22), na Uasin Gishu (11).