• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Mpango wa Charlene Ruto kusaidia kuzima uhuni Pokot Magharibi 

Mpango wa Charlene Ruto kusaidia kuzima uhuni Pokot Magharibi 

NA OSCAR KAKAI.

VIJANA katika Kaunti ya Pokot Magharibi, wanatarajiwa kunufaika kutokana na mpango maalum kuwapa ushauri nasaha kuhusu athari za pombe, mihadarati, mimba na ndoa za mapema.

Mpango huo unaoendelezwa chini ya wakfu wa SMACHS unaofadhiliwa na bintiye Rais William Ruto, Bi Charlene Ruto, pia unalenga kusaidia kupunguza visa vya uhalifu na ujangili katika kaunti.

Bi Charlene, anashirikiana na Wakili Kevin Kachapin, wakiwa na lengo la kuinua vijana wabadilishe mtazamo wao kimaisha na kukumbatia shughuli zitakazowanufaisha.

Aidha, wanalenga matineja shuleni kuwapa mashauri kupitia majukwaa yasoka.

Kijana Boaz Kiptoo kutoka mji wa Kapenguria ambaye alikuwa raibu wa pombe na dawa za kulevya anasema kuwa ni mwanzo mpya kwa vijana eneo hilo.

“Mimi nimeasi pombe na mihadarati baada ya kupata ushauri. Nimeanza kucheza soka,” anasema.

Mbinu hiyo, Bi Charlene anaitumia Pokot Magharibi kuteka vijana wakome kujiingiza kushiriki maovu na pia kukuza talanta zao kisoka.

Kiptoo alisema hayo baada ya kushiriki mchuano kati ya Keringet FC na Kamorro FC. Timu ya Keringet iliicharaza Kamorro bao 1-0.

Mchuano huo uliandaliwa katika uga wa Makutano mnamo Ijumaa, Machi 22, 2024.

Keringet FC ilituzwa Sh15, 000 pesa taslimu, na Kamorro FC ikipata Sh10, 000.

Bi Charlene ambaye alikuwa mgeni wa heshima kwenye mashindano hayo aliwataka vijana wa maeneo ya wafugaji kuzamia soka.

“Talanta zitabuni nafasi za kazi na kukupeleka mbali,” alihimiza vijana.

Kushiriki kandanda, Charlene alisema wametambua ni baadhi ya michezo iliyosahaulika eneo hilo na ikikumbatiwa inaweza kuwa ajira kwa vijana.

Watapalilia talanta, hivyo basi kuwapa mkate wao wa kila siku kujiendeleza kimaisha.

“Tunataka kuinua vijana eneo hili la mashinani ambalo linakumbwa na changamoto nyingi za ukeketaji, mimba za mapema na watoto wa kike kuozwa mapema,” alisema.

Vilevile, alitahadharisha wasichana wadogo kuhusu athari za mimba, ndoa za mapema na ukeketaji, akisema atajituma kuungana na wadauhusika kuweka mikakati maalum waweze kukata kiu cha elimu.

“Msikubali wavulana wawadanganye. Watakuwacha pekee yako,” alionya.

Kevin Kachapin ambaye ni mwanawe Gavana wa Pokot Magharibi, Bw Simon Kachapin, naye aliwataka vijana katika maeneo ya wafugaji kuzamia michezo kama njia mojawapo kunoa talanta ili kujiepusha na maovu.

Bw Kevin aliwataka vijana kujiepusha na mihadarati.

“Matineja ambao wanatumia mihadatari wakiwa bado wangali shuleni hawawezi kufaulu. Pokot Magharibi kuna umaskini mkubwa, na njia pekee ya kuuondoa ni kusoma,” alisema.

Afisa kutoka Idara ya Michezo katika Serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi, Bw Edwin Pkemei Lokomol alielezea imani yake kwamba kwa kushirikisha vijana kwenye soka, hatua hiyo itasaidia kupunguza matumizi ya dawa na mihadarati.

  • Tags

You can share this post!

Mwanaharakati atoka mafichoni kuendelea kutetea maskini

Tahadhari: Samaki kuwa adimu, mazingira Ziwa Victoria...

T L