Mpango wa upanuzi wa feri waibua wasiwasi Mombasa
MPANGO wa serikali kufanya upanuzi wa miundomsingi katika kivukio cha feri Likoni, Kaunti ya Mombasa, umeibua wasiwasi kwa wafanyabiashara kivukoni wanaohofia kufurushwa.
Wahudumu wa matatu, wachuuzi na wauzaji katika sehemu hiyo wametaka Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) kueleza wazi mipango ya kuwahamisha kupisha mradi wa uboreshaji wa kivuko hicho.
Wadau hao wanasema hawakuhusishwa kwenye kikao cha kwanza cha mashauriano kilichofanyika wiki iliyopita, licha ya wao kuwa miongoni mwa watakaoathirika moja kwa moja.
Wanahofia kuwa, maisha yao yataharibika endapo mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka miwili utaanza bila mpango rasmi wa kuwahamisha au kuwalipa fidia.
“Tuliambiwa kikao cha kwanza kilihusisha wote watakaoathirika, lakini sisi hatukualikwa. Badala yake walileta watu wengine wakidai kutuwakilisha. Jambo la kushangaza ni kuwa Meneja Mkuu wa Kenya Ferry anatufahamu vizuri. Kwa nini awaruhusu watu wasiohusika wazungumze kwa niaba yetu?” akauliza Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu, Bw Abdallah Kadi.
“Tumechukua magari kwa mikopo. Tukifurushwa bila mpango, tutaenda wapi? Kwa miaka zaidi ya kumi tumechangia zaidi ya Sh1.2 milioni kila mwezi katika uchumi wa eneo hili. Hatustahili kutelekezwa hivi,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa eneo la Baraka, Bw Bakari Nyanje, alisema wafanyabiashara zaidi ya 3,000 wanawakilishwa na chama chao lakini vioski vilivyotengwa ni 900 pekee, idadi aliyosema haitoshi hata kidogo.
Mwenzake wa Muungano wa Wamiliki wa Vibanda Likoni, Bw Salim Rashid, alisisitiza kuwa, suluhu ni kuhusishwa kikamilifu na kupewa nafasi mbadala ya kuendesha biashara.
“Kila mradi ukianza huwa tunaelewana, tunahamia upande mmoja huku mwingine ukikarabatiwa. Hilo ndilo tunatarajia pia. Isipokuwa hivyo, tuko tayari kwenda mahakamani,” akasema Bw Rashid.
Mfanyabiashara, Bi Pamela Muyangu, pia alieleza masikitiko yake kuhusu ukosefu wa maelezo rasmi kuhusu mustakabali wao.
Naibu Kamishna anayesimamia Kaunti Ndogo ya Likoni, Bw Mathew Wambugu, aliwataka kuwa watulivu akiahidi kwamba hakuna mtu atakayehamishwa bila mashauriano ya kina na mpango mbadala.
“Hadi sasa tumefanya kikao cha awali tu na viongozi pamoja na wataalamu. Hatua inayofuata ni kukutana na watu wanaoathirika moja kwa moja kisha tutafanya baraza la wazi kwa wananchi wote kutoa maoni yao,” alisema Bw Wambugu.
Aliongeza kuwa, ujenzi huo huenda usianze mwezi ujao au hata mwaka huu kwani bado upo katika hatua ya kupangwa.
Upanuzi unatarajiwa kuanza upande wa bara wa Likoni na utaendelea kwa muda wa miezi 24, kwa mujibu wa KPA.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA Kapteni William Ruto, kupitia hotuba iliyosomwa na Meneja Mkuu wa Kenya Ferry Bakari Gowa, alisema mradi huo unalenga kuboresha heshima na hadhi ya wasafiri wa kila siku.
Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko, alisema mradi huo umechelewa sana na unahitajika kwa dharura ili kuimarisha usalama.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Bw Mohamed Noor Hassan, aliunga mkono mpango huo akisema umezingatia watu wenye ulemavu na usalama wa waenda kwa miguu.
KPA imeahidi kufanya baraza la wazi kwa wakaazi wote wa Likoni kabla ya utekelezaji wa mradi kuanza rasmi.