• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Mradi wa choo na Wi-Fi wapingwa Mukuru-Fuata Nyayo

Mradi wa choo na Wi-Fi wapingwa Mukuru-Fuata Nyayo

NA SAMMY KIMATU

MRADI wa serikali unaonuiwa kupiga jeki vijana kimapato na kufaidi zaidi ya watu 20,000 katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo katika tarafa ya South B huenda ukakosa kufaulu baada ya kundi la watu kuupinga na kusababisha hali ya vuta nikuvute.

Akiongea na Taifa Leo mnamo Alhamisi, Naibu Kamishna katika Kaunti ndogo ya Starehe John Kisang alisema uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa jengo la kisasa lililo na afisi ya chifu na chumba cha kutoa huduma za mitandao na choo spesheli umesitishwa kwa wakati usiojulikana.

Aidha, mradi huo ulinuiwa kuzinduliwa katika uga wa Kanu ambapo awali kulikuwa na afisi za Kanu wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa pili wa Kenya, hayati Mzee Daniel Toroitich Arap Moi.

Bw Kisang aliongeza kwamba ukikamilika, ulikuwa ukabidhiwe kundi la vijana liitwalo Nairobi South Youth Network.

Bw Kisang alisema kwamba mradi huo umefadhiliwa na kampuni ya Athi Water ukilenga kufaidi zaidi ya watu 20,000.

Vilevile, Bw Kisang alisema serikali inatumia wizara ya vijana kuufanikisha mradi huo kwa kuweka mtandao wa Wi-Fi ili kutoa huduma za mikahawabwaka na e-Citizen.

“Serikali kupitia Wizara ya Vijana inaweka Wi-Fi ili vijana wahudumie wakazi kwa kutoa huduma za mitandao kupitia Cyber na masuala ya E-Citizen ambayo serikali inatilia mkazo kukumbatiwa na kila mkenya,” Bw Kisang asema.

Licha ya kila juhudi kufanywa ili kufanikisha mpango huo, Bw Kisang aliambia Taifa Leo kwamba kuna kundi pinzani linaloongozwa na Bw Patrick Mwangi linalotumia kila juhudi kuona na kuhakikisha ni mradi ambao unasambaratika.

Aliongeza kwamba kundi hilo, japo ni la wazee wala sio vijana, linadai halikuhusishwa ilhali hao ndio walianzisha majengo katika eneo hilo wakiwa viongozi katika utawala wa Kanu.

“Bw Mwangi na wenzake wanadai ni lazima mradi huo usitishwe kwanza. Pia wanadai, mradi huo ubadilishwe ili ukabidhiwe kundi lake badala ya vijana eti hao ndio wanafaa kulengwa kwa tetesi hao ndio walianzisha mtaa huo kupitia uongozi wa Kanu,” afisa huyo wa utawala akasema.

Kadhalika, Bw Kisang alishangaa kwamba mtaa wa Fuata-Nyayo uko nyuma kimaendeleo kwa sababu ya siasa za watu wachache.

“Ajabu ni kwamba huu ndio mtaa wa kipekee katika mitaa mingine ya mabanda iliyoko Starehe ambao hauna hata choo kimoja cha umma kuwafaa wakazi,” Bw Kisang akasema.

Hatimaye, alishauri wakazi kuwa na subira wakati serikali inafanya juhudi za kutatua mzozo huo na kusisitiza sharti watu wazingatie kukumbatia na kuheshimu sheria.

“Yeyote atakayechangia kwa njia moja au nyingine kusababisha maandamano, fujo au uharibifu wa mali atakabiliwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria”, Bw Kisang akaonya.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mvulana auawa kwa kupigwa risasi na majangili Pokot...

Zuchu sasa amtema Diamond, aahidi kumakinikia kazi WCB

T L