Msamaha wa mbunge kwa walimu Kisumu wakataliwa
MBUNGE wa Kisumu Mashariki Shakeel Shabbir ameomba msamaha baada ya kulaumiwa kwa kudhulumu walimu wakati wa shughuli moja katika shule moja ya upili katika eneo bunge lake wiki jana.
Bw Shabbir aliungama kuwa aliwakaripia, kwa maneno makali, walimu wa Shule ya Upili ya St Peter’s Kindu “baada ya kupandwa na hasira.”
“Nilipandwa na hasira, lakini lengo langu ni kuinua viwango vya elimu. Kwa kila mwalimu aliyehisi kudhalilishwa, naomba msamaha,” akasema.
Hata hivyo, vyama vya kutetea masilahi ya walimu vimepuuzilia mbali msamaha huo vikisisitiza kuwa sharti autoe rasmi na moja kwa moja kwa walimu wahusika na walimu wote kwa ujumla.
Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) na Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) sasa vinapendekeza kuhamishwa kwa walimu wote kutoka shule hiyo, wakitaja mazingira mabaya ya kufanyia kazi.
“Tunatangaza rasmi kwamba Shule ya Upili ya St Peter’s sio salama kwa walimu. Tunaitaka Tume ya Huduma za Walimu kuwahamisha walimu wote kutoka shule hiyo kwa usalama na heshima yao,” akasema Katibu Mkuu wa Kuppet, Bw Akelo Misori, kwenye kikao na wanahabari mjini Kisumu.
Kero za Kuppet zinatokana na kisa cha Ijumaa wiki jana ambapo Bw Shabbir aliwashambulia kwa maneno makali walimu wa Shule ya Upili ya St Peter’s Kindu, akiwalaumu kwa matokeo mabaya.
Mbunge huyo aliwasuta walimu hao wakati wa mkutano wa wazazi na wanafunzi.
Katika video iliyosambazwa mitandaoni, Bw Shabbir, ambaye alikuwa mgeni wa heshima, anaonekana akiwazomea walimu kwa uzembe akitishia kuwafuta kazi na kuajiri walimu wengine wasio na ajira.
“Nataka kujua saa ambayo ninyi hufika shuleni. Nitaweka mtu hapa wa kufuatilia mienendo yenu. Wazazi, nawaomba mnipe kibali cha kuwafukuza,” Bw Shabbir akasema katika video hiyo.
Hali ilikuwa mbaya zaidi pale Mbunge huyo alipomteua mwalimu mmoja wa kiume na kumrushia matusi kwa kusimama visivyo.
Walioshuhudia kisa hicho walisema mwalimu huyo aliingiwa na woga kwa kuzomewa mbele ya hadhira iliyojumuisha wanafunzi wake.