• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 8:50 AM
Mshonaji viatu atoa ardhi ya kujengwa shule

Mshonaji viatu atoa ardhi ya kujengwa shule

NA MAUREEN ONGALA

UMASKINI mkubwa unaoendelea kuwakumba wenyeji na wakazi wa Kaunti ya Kilifi umechangia pakubwa katika changamoto zinazoikumba sekta ya elimu.

Wazazi wengi wanashindwa kumudu karo za watoto wao na ada nyinginezo za kufanikisha elimu.

Hali hii imechangia watoto wengi kuendelea kukosa masomo yao kwa sababu ya kufukuzwa mara kwa mara.

Hata hivyo, katika jitihada za kutafuta suluhu kwa baadhi ya changamoto katika sekta ya elimu, mwanamme mmoja, ambaye ni fundi wa viatu katika soko la Tezo, amejitolea kukata na kupeana sehemu ya shamba lake kwa ujenzi wa shule.

Bw Jackson Kombe,51, alisema kuwa aliamua kutumia nafasi hiyo ya kipekee baada ya shirika la Gapeka Children’s Hope Centre kujitolea kusaidia watoto maskini kupata elimu.

Mzee Jackson Kombe akizungumza na wanahabari katika kipande cha shamba ambapo ujenzi wa shule ya Tezo Bright Academy unaendelea. PICHA | MAUREEN ONGALA

Shirika hilo lisilokuwa la serikali liliamua kuchukua shule ya kibinafsi ya msingi ya Tezo Bright Academy kufuatia ombi la mwanzilishi wake,  Mchungaji Riziki Morris wa Kanisa la St Peters Brain of Life na jamii ya Tezo kuiendeleza na kuwapa wanafunzi maskini mandhari mazuri ya kusoma ili kutimiza ndoto zao za kielimu.

Wanafunzi katika shule hiyo wanapitia changamoto nyingi, ambazo ni pamoja na ukosefu wa vitabu na kalamu kwani wazazi wao hawana uwezo wa kununua.

Mandhari ya shule hiyo hayajakaa vizuri sana kwani watoto hao wanaendeleza masomo yao katika jengo moja ambalo linaonekana kuwa gofu lilojengwa kwa minajili ya kuwa na vyumba vya kukodisha ambalo halikuwahi kukamilishwa.

Halina madirisha, milango wala sakafu kulainishwa vizuri.

Akizungumza na wanahabari mjini Tezo, Bw Kombe alisema kuwa licha ya kuwa watoto wengi wana hamu ya kuenda shuleni, umaskini umekuwa kikwazo kikubwa wasijue wakimbilie wapi kupata msaada.

“Nimeathirika pakubwa na umaskini ambapo watoto wangu wamekuwa wakifukuzwa shuleni kila mara kwa sababu sijalipa karo na wao huketi nyumbani kwa zaidi ya majuma mawili huku nikitafuta pesa,” akasema Bw Kombe.

Alieleza kuwa hali hiyo waliokuwa wanapitia watoto wake ni sawa na wanayopitia maelefu ya watoto kutoka familia maskini katika eneo la Tezo na sehemu nyingine katika Kaunti ya Kilifi.

“Nimetoa shamba hili kwa roho safi na sijawahi kujuta kwa sababu elimu ni muhimu na watoto wengi wana hamu ya kukata kiu ya elimu lakini wanakosa nafasi hiyo kwa sababu ya ukosefu wa karo,” akasema.

Bw Kombe alieleza kuwa alitoa kipande hicho cha shamba kwa masharti kuwa kila mtoto atakayejiunga na shule atasoma bila kutozwa karo.

“Watoto wangu pia wamepitia changamoto hiyo, mara wawe shule mara nyumbani lakini ninataka jamii yote ipate elimu bora na wapatikane shule wakati unaofaa,” akasema.

Fundi huyo wa viatu alieleza kuwa kiwango cha elimu katika eneo la Tezo kinazidi kuzorota kila mwaka huku watoto wengi wakilazimika kukatiza masomo yao kwa sababu ya kutokuwapo uwezo wa familia zao kuwalipia karo.

“Mtoto atafukuzwa na akae nyumbani wiki nzima, aende shuleni na kufukuzwa tena. Inakuwa changamoto kubwa kwa sababu hawapati elimu kwa muda unaofaa,”akasema.

Wakazi wa Tezo wanategemea ukulima na ufugaji wa mbuzi na ng’ombe ambapo hali huwa ngumu wakati wa kiangazi.

Alisema hapo mwanzo, alikuwa mkulima hodari kabla ya kuacha kazi hiyo na kuanza kushona viatu kwa miaka mitatu sasa.

Kwa sababu ya kipato kidogo kinachotokana na kazi ya yake, aliamua kuanza kuuza maziwa ya ng’ombe kuongezea pato lake la kila siku ili kukimu mahitaji ya familia yake.

Bw Kombe alisema kuwa hupata Sh400 au Sh300 kila siku kwa kushona viatu.

“Mimi sikusoma na hutegemea kushona viatu ili kulea familia yangu. Ndio maana ningependa kuona jamii yangu ikibadilika kupitia elimu,” akasema.

Mchungaji Riziki kwa upande wake alisema alianzisha shule hiyo mnamo Oktoba 2021 na wana watoto wanane ambao walikuwa nyumbani licha ya umri wao wa kuenda shuleni ulikuwa umewadia.

“Watoto hao walikuwa na changamoto mbalimbali. Baadhi yao ni mayatima, watoto wanaolelewa na mzazi mmoja, na wengine ambao wazazi wao ni wa kipato cha chini mno,” akasema Bi Riziki.

Alieleza kuwa amri ya serikali ya kitaifa ya kutaka machifu na askari kuwakamata wazazi na watoto wao ambao hawaenda shuleni iliwatia wazazi wengi hofu wasijue la kufanya kwani wengi wao hawakuwa na karo.

Hapo ndipo wengi wa wazazi hao waliwapeleka watoto wao katika shule hiyo ambapo wakati huo ilikuwa kanisani.

“Watoto wote waliokuwa nyumbani walikuwa wanashikwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Ngerenya na wazazi waliposikia nimefungua shule kwa kanisa, wakaleta watoto hao ambao walikuwa katika viwango tofauti ngazi ya elimu,” akasema.

Hali hii ilikuwa changamoto kubwa kwake kwani ilimlazimu kuwafunza watoto hao kulingana na kiwango chao.

Idadi hiyo iliongezeka kwa kasi na kufikia watoto 200 na hali ikazidi kuwa ngumu kwa Kanisa kwani maafisa wa elimu waliingilia kati kumtaka awe na mazingira bora kwa watoto hao kusomea.

“Ilikuwa vigumu kwa sababu wakati nafunza darasa moja wanafunzi wa darasa lile jingine wanaacha kufanya kazi zao na kuanza kunisikiliza,” akasema.

Ilimbidi kukodisha jengo hilo ambalo alikuwa analipa kodi ya Sh1,500 kwa kila chumba.

“Wanafunzi walizidi kuongezeka na wazai hawana uwezo, ndiposa nikaamua kutafuta ni vipi watoto hawa wangesaidika kusomea katika mazingira bora na kupata mahitaji yao yote,” akasema.

Hata hivyo, alichukua hatua ya kubaki na watoto wa shule ya chekechea pekee ili kupunguza changamoto.

Afisa mkuu mtendaji wa Shirika la Gapeka Children’s Hope Centre Jonathan Guyo alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo ya Tezo Bright Academy katika kipande hicho cha shamba utagharimu Sh9 milioni.

“Baada ya kuombwa msaada na jamii ya Tezo, tulifatilia na mwishowe tukaafikia makubaliano ya kushirikiana ili kuuchukua na kuuendeleza. Hivi sasa wanafunzi wako katika majengo duni sana ambayo hayastahili kuwa madarasa,” akasema Bw Guyo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Gapeka Children’s Hope Centre Bw Jonathan Guyo akihutubia wanahabari ofisini mwake mnamo Februari 5, 2024. PICHA | MAUREEN ONGALA

Bw Guyo alisema wanalenga kuendeleza shule hiyo ya chechekea hadi kufikia kiwango ya shule ya msingi na wanafunzi kutoka hapo watajiunga katika shule ya upili ya The Great Vonwald chini ya usimamizi wa shirika hilo.

Ujenzi wa shule ya Tezo Bright Academy unatazamiwa kukamilika Juni 2024 na kufunguliwa rasmi.

Bw Guyo alisema wanalenga kufadhili watoto 500 kutoka kwa familia maskini katika eneo la Tezo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wanawake Lamu wadai ladha ya ndoa ni ‘kuwakalia...

Men’s Conference: Kongamano la mashambulizi shtukizi ya...

T L