Msichana aliyeuawa na majangili azikwa kijijini Karawali
NA OSCAR KAKAI
MSICHANA wa umri wa miaka saba aliyeuawa na majangili katika eneo la Kamologon, Kaunti ya Pokot Magharibi wiki jana amezikwa, wakazi na viongozi wakitaka haki kutendeka.
Pia wanataka askari wa akiba na wanajeshi kutumwa kwa wingi kuimarisha usalama katika eneo hilo.
Wakihutubu katika hafla ya mazishi Jumatano jioni, baadhi ya wakazi na viongozi waliopewa nafasi walisuta vikali maafisa wa usalama wanaohudumu katika eneo hilo kuhusu kuzembea kazini na kukosa kufika wakati kukiwa na mashambulio.
Walisema kuwa akina mama na watoto wamekuwa wakilengwa kwa urahisi na wako kwenye hatari ya kuvamiwa na majangili ambao hujificha kwenye misitu.
Jumatano jioni, hali ya majonzi na huzuni iliwakumba wakazi kwenye kijiji cha Karawali, eneo la Kamologon kaunti ndogo ya Pokot Kusini kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet ambapo msichana huyo Shirleen Juliasia alizikwa.
Msichana huyo mdogo aliuawa na majangili akiwa na wenzake watatu wakichunga mifugo ya wazazi wao.
Majangili hao pia waliiba mifugo kadhaa lakini baadaye ilirejeshwa.
Hali ya taharuki inaendelea kutanda huko, huku viongozi wa eneo hilo wakitaka fidia kulipwa kwa familia ambayo imeathirika.
Kulingana na wakazi, maafisa wa usalama huwa tu wanazuru eneo hilo mara moja kwa kipindi kirefu.
Mwakilishi wa wadi ya Tapach Samuel Korinyang alisema kuwa kwa muda mrefu, maafisa wa usalama wa eneo hilo hawajakuwa tayari kufanya kazi na kuitaka Wizara ya Usalama wa Ndani kuwapa uhamisho.
“Tumelia kwa muda mrefu kuhusu maafisa wa eneo la Kamelei kuenda kuishi Kapusheni. Huwa hawasikia milio ya risasi. Wao huchukua takriban saa sita kufika hapa. Wanapata majangili tayari wameua watu na wameiba mifugo na kutoroka,” alisema Bw Korinyang.
Mkazi Mama Brian Alfred alisema kuwa maafisa wa usalama wanaohudumu eneo hilo hawajasaidia jamii hiyo ipasavyo.
“Tunataka haki kwa familia. Serikali imefeli kwa kutotulinda. Akina mama na watoto wanalengwa,” alisema.
Mwezi mmoja uliopita, magavana kutoka jamii hasimu, kaunti za Pokot Magharibi, Baringo na Elgeyo Marakwet walifanya mkutano katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet kutafuta suluhu kuhusu ujangili.
Mwakilishi wa wadi ya Weiwei David Moiben alisema kuwa kuna haja ya kuweka kamati za amani kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet.
“Kuna kamati ya amani upande wa Pokot lakini upande wa Elgeyo Marakwet hakuna kamati,” alisema Bw Moiben.
Kamologon imegeuzwa eneo la maficho ya majangili ambao hutekeleza maovu.
Haya yanajiri huku visa vya mashambulio na wizi wa mifugo vikichipuka upya eneo hilo.
Wiki mbili zilizopita, majangili walivamia kijiji cha Sorewo katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, kilomita mbili tu kutoka penye aliyekuwa Mkuu wa Majeshi (CDF) Jenerali Francis Ogolla aliaga dunia baada ya ndege kuanguka eneo la Sindar.
Majangili hao pia waliiba mifugo 15 lakini ilirejeshwa na maafisa wa usalama.