Habari za Kaunti

Mung’aro aagiza kufungwa kwa chekechea zote Kilifi kufuatia kimbunga IALY

May 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WINNIE ATIENO

GAVANA wa Kilifi Gideon Mung’aro amefunga shule zote za chekechea kaunti hiyo kufuatia kimbunga hatari ya IALY baada ya upepo kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja.

Bw Mung’aro pia amepiga marufuku uvuvi ndani ya Bahari Hindi katika ngome zote za kaunti yake hadi pale hali ya hewa itatulia na kurejea ya kawaida.

“Tumekumbwa na ajali kutokana na upepo mkali unaovuma eneo la Pwani. Vigingi vya nyaya za nguvu za umeme vimeanguka na pale Mariakani paa la shule moja ya chekechea liling’oka na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja na wengine wanne kujeruhiwa vibaya,” akasema Bw Mung’aro.

Alisema kuanzia Alhamisi, shule zote za chekechea zisifunguliwe hadi wiki ijayo.

Vilevile aliagiza watoto wasiruhusiwe kukaa karibu na shule. Aliwataka wakuu wa elimu katika kaunti yake kuwatumia wazazi wote jumbe fupi (SMSs) kuwaarifu kuhusu kufungwa kwa shule hizo hadi wiki ijayo.

Akihutubu mjini Kilifi, Bw Mung’aro alisema kimbunga IALY kimesababisha uharibifu mkubwa hasa katika kaunti yake.

Alisema katika ofisi ya Huduma Centre, eneo la kuegesha magari limeathirika baada ya magari kuangukiwa na vigingi vya nyaya za umeme. Alisema eneo la Takaungu pia limeathirika baada ya miti kuangushwa na upepe huo unaovuma kwa kasi.

Alisema shule nyingine ya chekechea huko Magarini pia imeharibika baada ya mabati kusombwa na upepo huo.

“Wale wavuvi, hakuna kwenda baharini mpaka wiki ijayo. Hatutaki maafa baharini. Kama ni chakula idara ya uvuvi iwapatie wavuvi chakula ili wasiendee baharini kujitafutia. Upepo utakuwa mwingi sana hii wiki… tujitahadhari,” aliongeza.