Mungiki wadaiwa kutesa, kuibia abiria Karatina
NA MWANGI MUIRURI
WAHUNI wanaofungamanishwa na kundi haramu la Mungiki sasa wanadaiwa kuteka nyara mji wa Karatina ambao ni ngome kuu ya Naibu Rais, Rigathi Gachagua.
Imeripotiwa kwamba wahuni hao hushika doria katika maeneo kadha ya mji huo hasa katika steji za uchukuzi na pia kwa madanguro.
Kwenye ripoti moja ambayo Taifa Leo imeona katika kituo cha polisi cha Karatina OB 18/08/05/2024, wahuni katika steji kuu ya Karatina walipora abiria Sh4,200 na simu ya thamani ya Sh1,300.
“Wahuni hao walinirukia tu baada ya kushuka kutoka kwa matatu. Walianza kunizungusha wakinielekeza kwa magari mengine ya uchukuzi lakini na katika vuta nikuvute hiyo, mmoja wa wahuni hao aliingiza mikono kwa mifuko huku wengine wakinishika mikono na wakanipora,” ripoti hiyo ya mlalamishi yasema.
Licha ya maafisa wa usalama kuagiza kwamba magari yote yawe yakielekezwa kwa steji na wahudumu walio na sare, hao wa Karatina wa kupora watu huwa hawavai unifomu.
Aidha, huogopwa sana na wamiliki wa matatu kwa kuwa wao ndio hutoa idhini za kuhudumu kwa barabara na kisha kuwatoza ushuru haramu.
Huwa wanatangamana kwa steji pamoja na waajiriwa wa sacco za uchukuzi.
“Hao ni serikali kivyao. Huwa wanaogopwa sana na kichinichini huwa tunawafahamu kama ‘jeshi ya kikundi cha mwenyekiti’ ama kwa lugha inayoeleweka upesi huku, ‘jeshi ya chairman’,” akasema mmoja wa waajiriwa wa magari ya uchukuzi katika steji hiyo.
Taifa Leo haikubaini upesi huyo mwenyekiti ni nani.
Wenyeji walisema kwamba vijana hao wa uhalifu kwa kutumia vitisho vya uvamizi na mauaji huweza kujiweka kwa riziki haramu ya kutoza sekta za ushuru na mapato yasioendea serikali na hatimaye kupora raia.
“Polisi huwa wanawavamia mara kwa mara na kuwakamata lakini baada ya muda, huwa tunawaona wamerejea. Wamekuwa kero na hata baya zaidi, kuupa mji wetu taswira ya uhalifu,” akasema Bi Cecilia Waguthii, ambaye ni mchuuzi sokoni Karatina.
Walisema kwamba washirika wote wa genge hilo ni vijana ambao wanajulikana kwa sura na majina lakini kwa kuwa huogopwa, hakuna kitu ambacho wenyeji wanaweza wakawafanyia.