• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:55 AM
Muuzaji wa gesi anyakwa kwa kuhatarisha maisha ya wakazi

Muuzaji wa gesi anyakwa kwa kuhatarisha maisha ya wakazi

NA SAMMY KIMATU

MTU mmoja alikamatwa kwa kudaiwa kuendesha kituo haramu cha kuuza gesi akijua ni kinyume cha cheria na kuhatarisha maisha ya wakazi ndani ya mtaa.

Akiongea na Taifa Leo mnamo Ijumaa, Naibu Kamishna katika Kaunti ndogo ya Starehe John Kisang alisema mitungi 36 ilitwaliwa katika msako huo.

Bw Kisang alisema msako huo uliongozwa na mkuu wa tarafa ya South B Solomon Muraguri akishirikiana na machifu, manaibu wa machifu na viongozi wa mtaa.

“Maafisa walivamia nyumba nambari 61 katika mtaa wa River Bank Phase One ambapo walipata nyumba hiyo ilikuwa imegeuzwa kuwa kituo cha kuuza gesi. Mshukiwa kwa jina Bw Harrison Kimani, 32 alitiwa baroni. Tulipashwa habari kuhusu biashara hiyo na wananchi baada ya wakazi katiaka mtaa huo kuhofia maisha yao yamo hatarini kufuatia kisa cha mkasa wa Embakasi ambapo lori ya kubeba gesi lililipuka na kusababisha maafa huku watu kadhaa wakiwachwa wakiuguza makovu baada ya kuchomeka viungo tofauti mwilini,” Bw Kisang akasema.

Aliongeza kwamba misako mingine inaendelea kulenga kuondoa uuzaji wa gesi katika maskani za watu ili kuepusha maafa mengine.

“Ni maagizo tunayotekeleza sisi wasimamizi baada ya kuamriwa na rais William Ruto kufanya hivyo,” Bw Kisang akaeleza.

Katika mchakato huo, maafisa hao walitwaa mitungi ya gesi iliyokuwa imewekwa chapa ya K-Gas, Afrigas, Rubis, Total, Standard, Raha na Mpishi miongoni mwa mingine.

Maafisa watwaa mitungi ya gesi mtaani South B kutoka kwa makazi wakishuku mmiliki alikuwa  akiendesha biashara haramu. Msako uliongozwa na mkuu wa tarafa ya South B Solomon Muraguri. PICHA | SAMMY KIMATU

Bw Kisang alisema wanamhoji Bw Kimani ili kuwawezesha kuwatia mbaroni wale wote wanaoshirikiana naye katika biashara hiyo.

Akijitetea, Bw Kimani aliambia Taifa Leo kwamba hakuwa akiuza gesi kutoka kwa nyumba bali alikuwa ana duka ambako huuzia gesi.

Alidai, alipatikana kama ameweka mitungi hiyo aliyodai alinunua siku moja kabla ya kukamatwa kwake akinuia kuipeleka katika duka anakouzia gesi saa za kukamatwa kwake.

“Mimi siuzi gesi kutoka kwa nyumba. Nilinunua mitungi hiyo na kuileta hapa. Sasa, nilipatikana nikiipeleka katika duka ambako ninafanyia kazi ya uuzaji wa mitungi pamoja na gesi,” Bw Kimani akasema akiwa amefungwa pingu mkononi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wito Serikali iwezeshe wakulima wadogo kutumia sola kwa...

Sababu za baadhi ya watu kuogopa giza

T L