Mwana wa bwanyenye akamatwa kuhusiana na mauaji ya mwanamke
MWANA wa mfanyabiashara tajiri amekamatwa kuhusiana na mauaji ya mwanamke ambaye mwili wake ulipatikana umetupwa kwenye tanki la maji taka katika mji wa Ngurubani, kaunti ya Kirinyaga.
Kwa mujibu wa ripoti, maafisa wa upelelezi waliomfuatilia kwa kutegemea taarifa kutoka kwa raia walimkamata mshukiwa Ijumaa mchana katika maficho yake eneo la Mwariko, eneobunge la Mwea, na kumpeleka katika kituo cha polisi cha Wang’uru kwa mahojiano.
Mwili wa mwanamke huyo, ambaye bado hajatambuliwa, uligunduliwa Jumamosi iliyopita na mfanyakazi aliyekuwa akisafisha choo katika hoteli moja mjini humo.
Inasadikiwa kuwa marehemu alinyongwa hadi kufa kisha mwili ukatupwa kwenye tanki la maji taka ili kuficha ushahidi wa uhalifu huo.
Kamanda wa polisi wa Mwea Mashariki, Bw Mohammed Jarso, alisema mshukiwa mkuu, ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu aliyeacha masomo, atafunguliwa mashtaka ya mauaji baada ya uchunguzi kukamilika.
“Hili ni kosa kubwa sana, na mshukiwa mkuu atakabiliwa na mashtaka ya mauaji,” alisema Bw Jarso.
Polisi walisema kuwa uchunguzi unaendelea kubaini sababu ya uhalifu huo na mahali marehemu alikuwa akiishi.
Tayari baba wa mshukiwa, amerekodi taarifa na anasaidia polisi katika uchunguzi.
Mfanyabiashara huyo aliitwa kwa mahojiano katika kituo cha polisi cha Wang’uru mara baada ya mwili wa marehemu kupatikana, ambapo alihojiwa kwa saa kadhaa na baadaye kuachiliwa.
Aidha, wafanyakazi wake watatu pamoja na mkewe pia walirekodi taarifa kwa polisi na kuachiliwa.
Inadaiwa kuwa mshukiwa alikutana na marehemu katika baa moja ya mtaa huo ambapo walianza kunywa pombe pamoja.
Baada ya kuzidiwa na ulevi, mshukiwa alienda na marehemu hadi nyumbani kwake. Baadaye, mwanamke huyo alipatikana amekufa ndani ya tanki la maji taka.
Maafisa wa upelelezi wanaamini kuwa mshukiwa alimpiga marehemu hadi kufa ndani ya nyumba yake usiku, kisha akavuta mwili wake hadi nje na kuutupa ndani ya tanki hilo kabla ya kutoroka.