Habari za Kaunti

Afisa wa kike atumia AK 47 kumpiga mumewe risasi 12 baada ya dhuluma, mahakama yaambiwa

Na TITUS OMINDE July 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

AFISA wa uchunguzi katika kesi ya mauaji inayomkabili afisa wa polisi wa kike anayedaiwa kumuua mumewe, aliaambia Mahakama Kuu ya Eldoret kwamba mshtakiwa alimpiga marehemu risasi 12.

Mahakama iliambiwa kwamba wanandoa hao walikuwa na mzozo wa mara kwa mara katika ndoa yao.

Koplo Stephen Nzau, kutoka DCI kaunti Ndogo ya Moiben katika ushahidi wake mbele ya jaji Reuben Nyakundi, alieleza kuwa uhusiano kati ya Lillian Biwott na mumewe aliyefariki Victor Kipchumba ulikuwa na doa na ugomvi.

Afisa Mpelelezi alisimulia jinsi Lillian, askari polisi wa utawala katika kitengo cha polisi wa miundombinu katika kaunti ndogo ya Turbo, aliomba uhamisho hadi kituo kingine ili kukaa mbali na mumewe ambaye alikuwa akimdhulumu kwa mazoea.

“Ripoti ya uchunguzi wa risasi imethibitisha kwamba mshtakiwa alimuua marehemu kwa risasi 12 papo hapo,” Bw Nzau aliambia mahakama.

Hata hivyo, Bi Biwott aliambia mahakama kuwa marehemu alikuwa akimshambulia mshtakiwa mara kadhaa na kumsababishia majeraha ya kila aina kutokana na ugomvi wa kinyumbani.

Bw Nzau aliambia mahakama kwamba kulikuwa na kisa kibaya ambapo marehemu alimvamia mkewe mbele ya wafanyakazi wenzake katika kituo cha polisi cha Ainabtich alikokuwa akiishi.

Bw Nzau alisema kuwa tukio hilo la kushambuliwa katika kituo cha polisi lilimfanya marehemu akamatwe na kufungiwa katika seli lakini wazazi wa wanandoa hao walingilia kati na kuomba aachiliwe kutoka rumande ili waandae njia ya upatanishi.

Akitoa ushahidi katika kesi hiyo, Bw Nzau aliambia mahakama kuwa Bi Biwott alitumia bunduki yake rasmi ya AK 47 kumpiga marehemu risasi.