Mwanamke aliyeolewa afurushwa kwa kupiganiwa na wanaume
NA MWANGI MUIRURI
KAMATI ya kiusalama katika Kaunti ya Murang’a kwa ushirikiano na wazee wa kijiji imemtimua mwanamke aliyezoea kupiganiwa na wanaume usiku.
Uamuzi huo uliafikiwa baada ya polisi kuitwa huku wanaume wawili wakivuruga amani ya umma kijijini usiku wa manane na akaagizwa akadishe nyumba mtaani.
“Ni kisa cha Kijiji cha Kang’ong’i kilichoko Kaunti ya Murang’a ambapo wanaume wawili walibishana kuhusu nani angeanza kula uroda na mama huyo anayesifika kwa kutega wanaume, bila huruma” akasema mdokezi wetu.
Mdokezi alisimulia kwamba kisanga kilizuka wakati wanaume wawili walijipata wakiwa na mama huyo nyumbani kwa mmoja wao mwendo wa saa sita na nusu lakini hawakuweza kuafikiana ni nani angetangulia kuchovya asali.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi iliyoandaliwa na Kamanda wa polisi wa Murang’a Mashariki Bi Mary Wakuu, tukio hilo liliishia kuvuruga amani huku wanakijiji wakijitokeza kushiriki maandamano usiku wa manane.
“Mwendo wa saa saba hivi usiku tulipata habari kuhusu vurugu katika kijiji hicho. Kutuma maafisa wetu tulikumbana na hali ambapo wanaume wawili wa umri wa ujana chini ya miaka 30 walikuwa wakivurugana wakibishania mahaba na mwanamke mmoja jirani,” Bi Wakuu akasema.
Baada ya kuhojiwa, wanaume hao wawili pamoja na mwanamke huyo walijieleza kwamba awali walikuwa katika baa moja wakibugia pombe na saa za kufunga zilipofika, wote watatu wakaafikiana waende kwa nyumba ya mwanamume mmoja wakarushane roho na mama huyo.
“Baada ya kufika kwa nyumba, balaa ilizuka wakati mwenye nyumba alisema yeye ndiye angekuwa wa kwanza kuchovya asali, mwingine akibishania nafasi hiyo huku mwanamke akiwaambia waelewane ili kazi ifanyike,” akaongeza.
Vurugu zilizotanda wanaume hao walipokosa kuelewana ndizo zilitoa majirani nje kuja kujua kulichotokea huku wengine wakipigia polisi simu.
“Baada ya kusikiliza kesi yao polisi waliafikiana kwamba hakukuwa na ukora wowote kwani wote watatu walikuwa watu wazima waliojipata katika mzozo wa kimapenzi. Na kwa kuwa hakuna yeyote alikuwa ametekeleza uhalifu wowote, polisi waliwataka wote watatu wadumishe amani na wakaondoka,” Bi Wakuu akaongeza.
Wanakijiji waliambia Taifa Leo kwamba mwanamke huyo huwa ananogesha biashara ya mahaba katika kijiji hicho na huwa maarufu sana kwa kuwa huwa wa bei nafuu.
“Bora tu umnunulie pombe yeye atakuwa wako kwa siku hiyo. Ana mume ambaye alifika mahali pa mzozo na akaambia polisi kwamba hana shida na mkewe kuwa katika mzozo huo wa kimahaba,” akasema Bi Jacinta Wangui, jirani.
Aliongeza kwamba mwenye nyumba alimkubalia mwenzake awe wa kwanza kuchovya asali ili awaondokee aende kwake na awaache sasa wawili hao na amani ya kujivinjari.
“Hii ni ile Sodoma ya Bibilia. Huku visa vya aina hii huwa ni vingi na huchochewa na viwango duni vya elimu, ukosefu wa itikadi dhabiti za dini takatifu, wingi wa pombe haramu na mihadarati pasipo kusahau umang’aa usio na mwelekeo,” akasema Bi Wangui.