Habari za Kaunti

Mwanamume atupwa jela miaka 20 kwa kulawiti mvulana jandoni

Na TITUS OMINDE October 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANAMUME mmoja kutoka Kaunti ya Uasin Gishu amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mvulana wa umri mdogo wakati wa sherehe za tohara ya kitamaduni msituni Kapseret mnamo Novemba 2023.

Amon Kaile almaarufu Kurukuru, alihukumiwa na Mahakama ya Eldoret kwa kosa la kulawiti mvulana huyo mara mbili ndani ya siku mbili, akidai kuwa ilikuwa sehemu ya “mafunzo ya kuwa mwanamume.”

Kwa mujibu wa mahakama, mshtakiwa alimdanganya mtoto huyo kuwa kitendo hicho kilikuwa sehemu ya sherehe za kitamaduni, na kwamba wavulana wengine waliopitia tohara pia walifanyiwa vivyo hivyo.

Mvulana huyo alieleza kuwa alilazimishwa kuvumilia mateso hayo huku akiambiwa kuwa iwapo angefichua siri, “mizimu wa mababu wa tohara” wangemlaani.

Tukio hilo lilifanyika ndani ya msitu wa Cheleban, ambapo Kaile alitarajiwa kuwa mlezi wa mvulana huyo jandoni.

Baada ya tukio hilo, mvulana huyo alieleza jirani aliyemwamini kuhusu kilichotokea, na uchunguzi katika Hospitali ya Moi ulithibitisha kuwa alidhulumiwa kingono.

Katika hukumu yake, Hakimu Mkuu Mwandamizi Mogire Onkoba alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka ulikuwa wa kutosha, na kwamba Kaile hakutoa ushahidi wa kuaminika.

“Watoto wana haki ya kulindwa dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote. Mahakama hii imeridhika kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa kisingizio cha tamaduni,” alisema hakimu.

Kaile alidai kuwa alisingiziwa na watu waliotaka ajiunge na dini yao, lakini mahakama haikushawishika na utetezi huo. Amepewa siku 14 kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.