Mwanaume akatwa mikono kwa kuiba ndama
MWANAMUME ambaye alipatikana na ndama aliokuwa ameibwa, alikatwa mikono na kujeruhiwa vibaya Jumamosi katika kijiji cha Kamachuku, eneo la Mitheru, Kaunti ya Tharaka-Nithi.
Mwanamume pamoja na wenzake wawili walikuwa wamevamia boma la James Kaburu na kuiba ndama huyo kabla ya Bw Kaburu kuwaona kisha akapiga nduru.
Washukiwa wengine wawili walitoweka huku mshukiwa akiandamwa na wanakijiji ambao wamelalamikia visa vya wizi wa mifugo eneo hilo.
Ni wakati wa kipigo hicho ambapo wakazi wakitumia silaha butu, walimkata mkono mmoja huku mwingine ukijeruhiwa vibaya.
Polisi walifika na kumwokoa mwanaume huyo ambaye umati ulikuwa ukitaka kumuua kisha wakampeleka Hospitali ya Chuka Level 5 ambapo anaaendelea kutibiwa.
Kulikuwa na kioja wakati ambapo umati ulimfanyia mshukiwa huyo huduma za kwanza kisha wakaanza kumhoji kuhusu mahali ambapo wamewahi kuiba mifugo kisha mahali ambako wao huwauzia.
Kando na kuyataja majina ya watu aliokuwa akiiba nao, alifichua kuwa walikuwa wakiwachinja mifugo hao kisha kuuza nyama yao kwenye kichinjio kimoja jijini Chuka. Pia walikuwa na buchari ya kuuza nyama kwenye soko la Ndagani.
Mkazi mmoja alisimulia kuwa amewahi kuibiwa kondoo wake wawili na kuku 100 ndani ya siku tano na hilo lilimfanya akome kabisa ufugaki.
“Inasikitisha sana kuwa wizi wa mifugo umekuwa ukinoga sana katika kijiji hiki. Hilo lilichangia kwangu kuacha ufugaji,” akasema Bw Kaburu.