Naibu Gavana atwaa uongozi kwa makeke akiahidi kusaidia Arati kupambana na ufisadi
NAIBU Gavana mpya wa Kisii Julius Obebo amesema kuwa malengo yake makuu yatakuwa ni kusaidia Gavana Simba Arati kupigana na ufisadi katika Kaunti hiyo.
Bw Obebo amesema kuwa kando na kuwa mwaaminifu kwa gavana, vita dhidi ya ufisadi lazima vifanikiwe katika kaunti hiyo ili kuhakikisha wananchi wana imani kwenye utendakazi wa kaunti.
“Nawahakikishia kuwa mtumishi mwema kwa bosi wangu. Pia, nitahakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za umma,” akasema Bw Obebo, 60, wakati wa kuapishwa kwake kama naibu gavana,
Jana, Jumatatu, Julai 22, 2024 alichukua wadhfa huo kutoka kwa mtangulizi wake Dkt Robert Monda, aliyeng’atuliwa mamlakani mnamo Machi 2024 na Bunge la Seneti.
Dkt Monda alipatikana na makossa ya matumizi mabaya ya afisi yake na sababu zingine tatu.
Hafla ya kuapishwa kwa Bw Obebo iliongozwa na maafisa kutoka Idara ya Mahakama na kushuhudiwa na Gavana Simba Arati, wageni waalikwa na raia wengine katika uga wa michezo wa Gusii.
Gavana Arati alimtaka msaidizi huyo wake kutokubali watu wa nje kuwagonganisha na alimwomba awe mwaminifu wanapowahudumia wakazi wa Kisii.
Gavana huyo alitanguliza kwa kudai kuwa baadhi ya watu (japo hakuwataja) walijaribu kuzuia jina la mteule huyo kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la kiserikali lakini Rais William Ruto akaingilia kati.
“Nataka kumshukuru Rais kwa kutusaidia. Kuna baadhi ya watu waliojaribu kuzuia jina la Bw Obebo kuwekwa kwenye gazeti la serikali lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tulifaulu,” akasema Bw Arati.
Kabla ya uteuzi wake kama naibu gavana, Bw Obebo alikuwa ni mwenyekiti wa Bodi ya Utumishi wa Umma na Uajiri wa Wafanyakazi wa Kaunti ya Kisii (CPSB).
Aliteuliwa naibu gavana miezi michache tu baada ya kuteuliwa mwenyekiti wa bodi hiyo.