Habari za Kaunti

‘Nashukuru Mungu kuwa hai’, ahadithia manusura wa ajali ya Miasenyi-Voi iliyoua 7

December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WATU saba walifariki na wengine 11 kujeruhiwa vibaya jana (Jumapili) asubuhi baada ya gari la usafiri wa umma (PSV) walilokuwa wakisafiria kugongana na lori katika eneo la Miasenyi, kwenye barabara ya Nairobi–Mombasa, Kaunti ya Taita Taveta.

Gari hilo lilikuwa likisafiri kutoka mjini Wote kuelekea Mombasa wakati ajali hiyo ilipotokea majira ya saa kumi na moja asubuhi. Majeruhi walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Moi mjini Voi kwa matibabu.

Afisa mkuu wa matibabu wa hospitali hiyo, Dkt Swaleh Khamis, alithibitisha kuwa watu saba walihamishiwa katika vituo vingine kwa ajili ya matibabu maalumu.

Alisema wengi wa wagonjwa walipata majeraha ya kuvunjika mifupa sehemu mbalimbali ingawa hali zao zilikuwa thabiti lakini zinahitaji uangalizi zaidi.

“Tumepokea majeruhi 11 kutoka kwa ajali ya barabarani. Kwa bahati mbaya, watu saba walitangazwa kufariki walipowasili. Wanne ni wanaume na watatu ni wanawake. Bado hawajatambuliwa,” alisema Dkt Khamis.

Aliongeza kuwa, hospitali hiyo imeruhusu wagonjwa wawili kurudi nyumbani na kumlaza mgonjwa mmoja wa kiume kwa uchunguzi zaidi.

“Mtoto aliyejeruhiwa kidogo amepewa matibabu na yuko chini ya uangalizi,” alisema.

Dkt Khamis alisema hospitali inajiandaa kwa uwezekano wa ongezeko la ajali za barabarani msimu huu wa sikukuu.

“Tunayafanya yote tuwezayo kujiandaa kwa msimu wa sikukuu. Tunaweka mikakati ya kukabiliana na idadi kubwa ya majeruhi iwapo itahitajika,” alisema.

Shahidi mmoja alisema baadhi ya majeruhi walikwama ndani ya matatu kwa dakika kadhaa kabla ya kupata msaada.

Mmoja wa manusura, Bi Agnes Mutunga, alisimulia tukio hilo la kutisha kabla ya ajali. Alikuwa amepanda gari hilo mjini Wote majira ya saa mbili usiku Jumamosi, akitarajia kufika Mombasa alfajiri.

“Tulisafiri usiku kucha. Nilikuwa nimelala nusu usingizi nilipohisi mshtuko wa ghafla kisha mlipuko mkali. Nilijikuta nimejeruhiwa, sikuweza kuzungumza au kusogea.”

Namshukuru Mungu kuwa niko hai,” alisema.

Bi Mutunga, ambaye alipata jeraha la jicho na mguu, alisema matatu hiyo ilikuwa ikijaribu kulipita gari lingine ilipogongana na lori lililokuwa likielekea upande wa pili.

“Ninaomba madereva wawe waangalifu barabarani. Nilikuwa nimeingiwa na wasiwasi kwa sababu dereva alikuwa akipita magari kwa kasi lakini nikalala usingizi na baadaye nikaamshwa na ajali,” alisema.

Katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, familia za marehemu zilikuwa bado hazijafika kutambua miili ya wapendwa wao.