• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Nassir atangaza makataa kwa wenye biashara zinazohitaji vibali

Nassir atangaza makataa kwa wenye biashara zinazohitaji vibali

NA FARHIYA HUSSEIN

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imetangaza makataa ya mwisho wa Januari kwa wale wenye deni la vibali vya biashara kwa mtu binafsi.

Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir alibainisha kuwa timu itaundwa kusimamia mchakato huo ili kuhakikisha deni lote limekamilishwa.

Alisema hatua hii ililenga kupunguza mzigo wa kifedha kwa wafanyabiashara katika kaunti hiyo, lakini pia kuimarisha mazingira ya kiuchumi yenye usawa.

Timu ya maafisa, alisema gavana Nassir, itakuwa ikitembelea maeneo mbalimbali ya jiji, kusuluhisha madeni yaliyosalia, na kuwahimiza wafanyabiashara walioko masokoni kulipa madeni yao.

“Watakuwa na kadi maalum wanapokuja. Kuwatambua unaweza kuipiga skani ili kuhakikisha wanatoka kwenye kaunti. Hivi ndivyo tunaweza kuepuka malalamiko,” alisema Bw Nassir.

Akaongeza: “Wale ambao hawajatekeleza na wameorodheshwa ni takriban 700 wakati wale waliofuata maagizo ni biashara 7,000,” alisema akiongeza kuwa riba inazidi Sh150 milioni.

Mkuu wa kaunti aliwahimiza wafanyabiashara kufuata nyakati zilizowekwa akitoa shukrani kwa wale ambao wamefanya hivyo.

Gavana Nassir alisisitiza usawa ndani ya jamii ya biashara, akidhihirisha umuhimu wa kila mwanachama kutimiza wajibu wao, kuhakikisha usawa.

“Haitakuwa haki ikiwa jirani yako analipa wakati wewe unakataa,” aliongeza.

Alisema kaunti inakabiliwa na changamoto za kutoa huduma katika masoko kutokana na michango isiyolingana, haswa katika ukusanyaji wa kodi za vibanda.

“Fedha zinazokusanywa kutoka kodi za vibanda ni chini ya Sh2 milioni kwa mwezi. Ndiyo sababu tuko katika mchakato wa kutangaza uendeshaji wa mifumo ya kiotomatiki katika malango ya kuingia masokoni ambapo tutakuwa na rekodi ya magari mangapi yalifika sokoni kwa siku,” alisema.

“Nia yangu si kutafuta utajiri kupitia kukusanya fedha hizi, bali ni kuhusu usawa na mafanikio ya Mombasa kwa ujumla. Mipango hufikia zaidi ya faida za kifedha, pesa hizi zinasaidia katika kufanikisha upatikanaji wa elimu, huduma za afya, na maendeleo ya miundomsingi mingi tu,” alieleza.

Mnamo Aprili 2023, Serikali ya Kaunti ya Mombasa iliongeza muda wa msamaha wa faini kwa wamiliki wa ardhi na wafanyabiashara kwa siku 30 kufuatia vikwazo vya kiuchumi.

Wamiliki wa ardhi walikuwa wamepewa hadi Machi 31, 2023, kulipa madeni yao lakini Bw Nassir ameongeza muda hadi Aprili 30, 2023, baada ya maombi kutoka kwa wakazi.

Gavana Nassir alisema alivutiwa na majibu kutoka kwa wamiliki wa ardhi ambao walitumia msamaha huo kulipa madeni yao ya ardhi yaliyokuwa yamejilimbikiza.

Gavana aliwapongeza wakazi kwa kuwa na imani katika serikali yake na ajenda ya maendeleo kulingana na ongezeko la Mapato ya Chanzo Cha Kitaifa kutoka kwenye akaunti za ardhi baada ya kutangazwa kwa msamaha wa adhabu zote.

  • Tags

You can share this post!

Majonzi kijana akitumbukia na kuangamia kisimani

Viongozi wa kidini washangaa vijana kulewa licha ya kulia...

T L