• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Nassir: Matibabu ya bure ni kwa watoto wa 001 pekee

Nassir: Matibabu ya bure ni kwa watoto wa 001 pekee

NA FARHIYA HUSSEIN

GAVANA wa Kaunti ya Mombasa Abdulswamad Nassir ametetea mpango wake wa huduma za matibabu ya bure unaowanufaisha watoto walio chini ya umri wa miaka mitano katika kaunti nzima.

Amejitokeza baada ya ripoti kuibuka kuwa baadhi ya wazazi walikuwa wanatakiwa kulipa huduma zilizotolewa kwa watoto wao, ingawa gavana alikuwa ametangaza kwamba ingekuwa bure.

Gavana Nassir amesema programu hiyo ni mahususi kwa ajili ya watoto kutoka kaunti hiyo na si wale wa kutoka nje ya Mombasa.

“Ukilitazama Hospitali ya Rufaa ya Pwani, asilimia 60 hadi 70 ya watoto wagonjwa huko si wa kutoka Mombasa. Tafadhali, nielezeni… ni wapi nitapata pesa hizi nitakapoanza kutoa msamaha kwa watoto wote wa pembe zote za Kenya?” aliuliza Bw Nassir.

Programu hiyo ilizinduliwa Mei 2023 ambapo gavana alisema utawala wake ungehakikisha watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanapata matibabu bure katika hospitali hiyo ambayo pia hujulikana kwa jina Coast General, na vituo vyake vya kutolea huduma ndani ya Mombasa.

Alitoa jibu kuhusu madai kwamba aliwafukuza wamiliki wa kampuni ya Mombasa Cement wasiendelee kutekeleza wajibu wao wa kifedha wa kuwalipia bili za hospitali baadhi ya wagonjwa maskini waliokwama hospitalini.

Gavana Nassir alisema mpango wake unafanikishwa na fedha zilizokusanywa kutoka sekta mbalimbali katika kaunti, akiongeza kuwa utawala wake ulikuwa unatumia Sh6 milioni kila mwezi kusaidia Coast General kwa matibabu ya wakazi wasio na uwezo wa kifedha.

“Rasilimali za Mombasa ni mali ya watu wa Mombasa. Sitajiepusha na hilo, na sitafanya jambo lolote kinyume na wanachostahili,” alisema.

“Unatarajia nifanyeje? Nibebe mzigo wa mtoto kutoka nje ya Mombasa na kuwaacha watoto wangu kwa sababu naogopa watu watasema?” kiongozi huyo akauliza.

Alisema Mombasa hupokea takribani Sh650 milioni kila mwezi kama mgawao wa usawazishaji kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Alibainisha kuwa pesa hizo hazitoshi ikizingatiwa kaunti ina deni kubwa la mishahara linalofikia takriban Sh530 milioni kila mwezi.

Kikatiba, alisema gavana, anapaswa kutenga Sh70 milioni nyingine kwa Baraza la Kaunti ya Mombasa.

Kile kinachosalia kinapaswa kuelekezwa katika miradi ya maendeleo na huduma katika kaunti nzima, alieleza.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yasikia kilio cha Ruto

Buda afokea kicheche aliyemtia presha ateme mkewe ili amuoe

T L