• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Ndani ya Hospitali ya Wanini Kireri Magereza iliyojengwa miezi tisa kama mimba

Ndani ya Hospitali ya Wanini Kireri Magereza iliyojengwa miezi tisa kama mimba

NA LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI ya Wanini Kireri Magereza Level 4 mjini Ruiru, ambayo ilifunguliwa wiki jana, italeta mabadiliko makubwa katika utoaji wa matibabu na huduma za afya.

Hospitali hiyo ilifunguliwa rasmi mnamo Mei 17, 2024, kwenye hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki na mwenzake wa Ulinzi Aden Duale.

Wakati huo mawaziri hao waliandamana na makatibu wawili ambao ni Dkt Salome Beacco katibu wa Idara ya Urejebishaji tabia na Bw Patrick Mariru ambaye ni Katibu wa Wizara ya Ulinzi.

Pia mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alikuwepo.

Hafla hiyo ilifanyika katika gereza kuu la Ruiru ambapo Kamishna Mkuu wa Magereza Brigedia mstaafu John Warioba ndiye alikaribisha maafisa hao wa serikali.

Waziri Kindiki alipongeza juhudi zilizofanywa na gereza hilo kwa kujenga hospitali ya kisasa ambayo ina vifaa vya hali ya juu.

“Tuna imani ya kwamba wafanyakazi wa idara ya magereza na familia zao watapata nafasi ya kwanza kutibiwa kwenye hospitali hiii,” alisema Prof Kindiki.

Hata hivyo, alisema idara hiyo ifanye mipango kuona ya kwamba hata wananchi wa kawaida wanapata nafasi ya kutibiwa hapo.

Alipongeza wanajeshi kwa kujenga hospitali hiyo kwa miezi tisa pekee.

“Hiyo ni kuonyesha ukakamavu uliopo katika idara ya ulinzi ambapo watazidi kushirikiana hivyo kutekeleza majukumu mengine ya kuwafaa Wakenya,” alisema Prof Kindiki.

Alisema hata wagonjwa wenye maradhi sugu wataletwa katika hospitali hiyo ambayo ina vifaa bora zaidi vya matibabu.

Bw Duale alipongeza kazi safi iliyofanywa na wanajeshi hao kwa kujenga hospitali hiyo kwa muda mfupi mno.

“Baada ya kuzunguka ndani ya hospitali, tumeshuhudia vifaa vya hali ya juu na bila shaka madaktari waliohitimu wataletwa hapo,” alisema Bw Duale.

Aliwashauri wakuu wa hospitali hiyo waweke hospitali hiyo kwa hali bora ya usafi kutokana na jinsi kiwango chake kipo.

Bw King’ara ambaye hospitali hiyo iko kwa eneobunge lake, alipongeza juhudi za serikali kujenga hospitali ya kiwango hicho katika eneo lake la uwakilishi.

“Nina furaha kuu kwa hospitali hii kujengwa eneo hili ambapo mipango ikikamilika, wakazi wa Ruiru na vitongoji vyake pia watapata nafasi kutibiwa hapa,” alisema Bw King’ara.

  • Tags

You can share this post!

Muungano wa viongozi kina mama kumpigania Gachagua

Kukatwa mguu hakujawa kikwazo kwa mhudumu wa bodaboda

T L