• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Ni Kiswahili kila Jumatano ndani ya Bunge la Mombasa

Ni Kiswahili kila Jumatano ndani ya Bunge la Mombasa

BUNGE la Kaunti ya Mombasa limepitisha mswada kuwa lugha pekee itakayotumiwa katika bunge hilo kila Jumatano ni Kiswahili.

Mswada huo pia umetilia mkazo utambuzi wa Kiswahili kama lugha rasmi na hivyo basi itumiwe zaidi kwenye mijadala bungeni.

Hii inamaanisha madiwani watakuwa wanatumia Kiswahili kwenye mijadala na mawasiliano rasmi katika bunge la kaunti.

Hatua hiyo ilichukuliwa ili kutambua lugha hiyo ambayo madiwani hao walitaja kudumisha tamaduni za wakazi na uwiano wa kitaifa.

Akiwasilisha hoja hiyo, diwani wa wadi ya Portreitz Fadhili Makarani aliitaka Bunge la Kaunti kuwezesha pia mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa madiwani wote na wafanyakazi wa bunge hilo ili kuboresha ustadi wao wa kusema na kuandika lugha hiyo ya kitaifa.

“Bunge liidhinishe kuanzishwa kwa kikao cha mashauriano ya kila wiki kila Jumatano asubuhi, kinachohusu mawasiliano na mijadala, kinachoendeshwa kwa lugha ya Kiswahili pekee,” alisema Bw Makarani, kwenye pendekezo lake ambalo lilipitishwa.

Vilevile, aliwataka madiwani kujumuisha tafsiri ya Kiswahili katika mijadala yao na miswada inayowasilishwa katika bunge la kaunti.

Kwingineko, diwani wa wadi ya Ramisi, Kaunti ya Kwale, Bi Hanifa Badi Mwajirani, ameelezea namna alivyoweza kuwapiku wapinzani wake 20 huku akiwasihi wanawake kujitosa kwenye limbi la siasa.

Bi Mwajirani ambaye ndiye mwanamke wa kwanza kuchaguliwa diwani katika Kaunti ya Kwale alisema licha ya changamoto kwenye siasa, ipo haja ya wanawake wengi zaidi kuingia ili kuongeza idadi yao bungeni.

“Nilipoingia ndani ya Bunge la Kaunti niliweza kuchaguliwa kama kiongozi wa walio wengi. Katika safari ya siasa nilianza kuteuliwa na chama cha ODM, nikahudumu katika bunge la pili la ugatuzi la Kwale, lakini baada nikaamua kugombea kiti cha Ramisi na kufaulu,” alieleza Bi Mwajirani, ambaye alichaguliwa kupitia chama cha ODM.

Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa afisa wa polisi katika idara ya jinsia alisema azma yake ya siasa ilianza zamani.

“Safari yangu ya siasa haikuwa rahisi mwanzo ilibidi niite na kuzungumze na familia yangu, hata hivyo wengine walikataa na wengine wakaniunga mkono,” alieleza kwenye mahojiano ya runinga.

Bi Mwajirani alisema hakukata tamaa kwa sababu lengo lake lilikuwa kuwa kielelezo bora kwa mtoto wa kike huko Kwale akaamua kuvalia njuga siasa.

Alisikitika akisema tangu ugatuzi miaka 11 iliyopita hakujawai kuwa na mwanamke aliyechaguliwa kwenye bunge la kaunti.

“Kwenye kampeni zangu hali haikuwa rahisi, mwanzo watu wlaikuwa wanazungumza wakiulizana kwa nini mtoto wa kike anasimama mbele ya wanaume, haijawai kufanyika,” alisema.

Hata hivyo, aliwafuata masheikh wa Kwale ambao walisimama naye na kutoa aya tofauti tofauti za Qur’an zinazoruhusu mwanamke kuongoza.

Alisifu muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya akisema umemsaidia sana katika safari yake ya kisiasa.

Katika Bunge la Kaunti, anahudumia kamati mbalimbali ikiwemo ile ya masuala ya kiuchumi na kifedha, afya na maji.

  • Tags

You can share this post!

JSC yashusha bakora kwa jaji Kullow, hakimu Wambugu

John Matara ashtakiwa kwa wizi wa mabavu, ubakaji

T L