PAA hatarini kukosa mtu Magarini baada ya mgombeaji kuitiwa kazi serikalini
SIASA za uchaguzi mdogo wa eneobunge la Magarini, Kaunti ya Kilifi, zimechukua mwelekeo mpya baada ya mgombeaji aliyetarajiwa kuwakilisha Chama cha Pamoja African Alliance (PAA), kufanyiwa mahojiano ya kazi serikalini.
Bw Michael Kingi, ambaye alikuwa mbunge wa eneo hilo tangu 2017 kabla ya kupoteza kiti hicho kwenye uchaguzi uliofutiliwa mbali wa 2022, aliorodheshwa na kufanyiwa mahojiano ya kuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) wiki iliyopita.
Chama cha PAA kinaongozwa na Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi, na kimekuwa kikisisitiza kitakuwa na mgombeaji kwenye uchaguzi huo licha ya kuwa ndani ya muungano wa Kenya Kwanza, ambapo chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) pia kinatarajiwa kuwa na mgombeaji.
Katibu Mkuu wa PAA, Bw Kenneth Kazungu, amesema iwapo Bw Kingi atapata nafasi ya kazi katika SRC, chama hakitakuwa na budi kuwa na mgombeaji mwingine.
“Kingi alikuwa mgombea kiti wa chama chetu na tulikuwa tumempa tiketi kwa sababu alikuwa miongoni mwa wale waliowasilisha kesi kortini kupinga uamuzi wa uchaguzi wa 2022,” akasema.
Bw Kingi aliibuka wa tatu katika uchaguzi huo alipokuwa anapigania nafasi hiyo kwa awamu ya pili baada ya kuchaguliwa mwaka wa 2017 alipomng’atua Harrison Kombe.
Bw Kombe, mwanachama wa ODM, ndiye alitangazwa mshindi 2022 lakini matokeo hayo yakafutiliwa mbali na mahakama ilipopatikana kulikuwa na dosari.
Chama hicho tayari kilitangaza Bw Kombe atapewa tikiti ya moja kwa moja kuwania katika uchaguzi mdogo.
Mwelekeo
Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, ambaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha ODM Kilifi hivi majuzi, alitangaza kuwa wanasubiri mwelekeo wa kinara wa chama hicho na rais William Ruto.
“Tuko tayari kuanza kampeni zetu kwa sababu tayari tuna mgombea wetu ambaye ni Harrison Kombe ila tunasubiri mwelekeo kutoka kwa viongozi wetu,” akasema.
Licha ya kuondolewa mamlakani na mahakama, Bw Kombe ameendelea kujitokeza na kujiunga na Bw Mung’aro na viongozi mbalimbali katika mikutano ya hadhara.
Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara nchini, Bi Aisha Jumwa, alitaka muungano wa Broad-based kumtoa mgombea kiti mmoja ambaye atapambana na yule wale wa upinzani unaoongozwa na Rigathi Gachagua.
Kulingana na Bi Jumwa, Chama cha UDA bado kinatarajia kumsimamisha Bw Stanley Kenga kwenye uchaguzi mdogo.
Bw Kenga aliibuka wa pili baada ya kushindwa kwa kura mbili na Bw Kombe.
Bw Nyambega Gisega ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha United Progressive Alliance (UPA) kinachohusishwa na aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani nchini Dkt Fred Matiang’i, alisema muungano wa United Opposition utachagua mgombea kiti atakayewania kiti hicho.
Vyama vingine vinavyotarajia kuwa na wagombeaji ni Democratic for Citizen Party (DCP), United Progressive Alliance (UPA), Roots Party of Kenya (RPK) na Wiper.
Hivi majuzi Kinara wa Roots Party of Kenya (RPK), Bw George Wajackoyah, alikita kambi katika Kaunti ya Kilifi akiendeleza kampeni za chama chake na mgombea kiti, Bw Karisa Hamad Chadi.
Alifungua rasmi ofisi cha chama hicho katika eneobunge la Magarini.
Hapo awali kinara wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, alimtawaza rasmi Bw Samuel Nzai kuwa mgombea kiti wa chama hicho katika uchaguzi huo mdogo.