Pepo wa mauti arudi Kisii watu 5 wa familia wakiuawa
MAUAJI ya watu watano wa familia moja katika kijiji cha Metembe, eneobunge la Nyaribari Masaba, Kaunti ya Kisii, Alhamisi usiku kwa tuhuma za uhalifu, yameibua kumbukumbu za tukio sawa lililotokea eneobunge la Bonchari zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Wakazi wanasema mauaji hayo yalipangwa kwa umakini mkubwa na kutekelezwa na kundi linalodaiwa kuwa la watu waliokuwa katika harakati za kulipiza kisasi, kufuatia mauaji ya kijana mmoja kijijini humo takriban mwezi mmoja uliopita.
James Babu Nyabuga aliuawa kwa kupigwa hadi kufa na wanaodaiwa kuwa wauaji wake.
Wakazi wa Metembe wanasema kuwa wiki moja baada ya mazishi ya Nyabuga, watu hao walijipanga, wakakamata jamaa wa washukiwa na kuwafunga kwa kamba kabla ya kuwaua.
Inadaiwa kuwa washukiwa wa mauaji ya Nyabuga walikamatwa na baadaye kuachiliwa, hali iliyoibua madai kuwa wazazi wao, miongoni mwa waliouawa, huenda walisaidia kuwaokoa kwa njia zisizo halali.
“Walikuwa wakiwaua mmoja baada ya mwingine, wakimwagia miili yao petroli kabla ya kuichoma moto. Hata mbwa waliokuwa wakijaribu kuwashambulia hawakusazwa, nao pia walimwagiwa petroli na kuchomwa,” alisema mkazi mmoja.
Mauaji haya yameibua maswali kuhusu usimamizi wa mfumo wa haki katika Kaunti ya Kisii, ambao kwa sasa unaonekana kupoteza imani ya wananchi.
Wengi wa waliouawa hawakuhusishwa moja kwa moja na uhalifu, bali waliuawa kwa sababu ya uhusiano wao wa kifamilia na washukiwa.
Wakazi wanasema vijana kutoka familia hiyo walikamatwa kufuatia mauaji ya Nyabuga lakini baadaye wakaachiliwa.
Kutokana na hasira kwa polisi kushindwa kuchukua hatua dhidi ya washukiwa, wakazi walijipanga na kutekeleza mauaji hayo ya kiholela ambayo yaliwashtua wakazi wa vijiji jirani.
Wakati wa mazishi ya Nyabuga, wakazi walitoa onyo kali kwa mamlaka kwamba wasingechukua hatua, basi wao wangechukua sheria mikononi mwao.
Afisa Mkuu wa Kaunti Ndogo ya Masaba Kaskazini, Jane Munene, alilaani mauaji hayo na kuyataja kama yasiyovumilika.
“Wananchi hawafai kuchukua sheria mikononi mwao. Tunawasihi washirikiane na serikali kutatua changamoto za kiusalama,” alisema Bi Munene.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi waliambia Taifa Leo kwamba juhudi zao za kushirikiana na serikali kukabili ongezeko la uhalifu zimegonga mwamba kutokana na kile walichokitaja kama ufisadi na uzembe wa polisi.
Kama ilivyotokea Bonchari miaka iliyopita, wanamgambo walivamia mashamba ya washukiwa, wakaharibu mazao, kukata miti, kuchoma nyumba na hata kuwaua mifugo waliowapata.
Waliouawa ni baba, mke wake, mwanawe, mjukuu, mkwe, na mpwa. Wengine waliolengwa walitoroka.
Kati ya 2003 hadi 2010, Bonchari ilijipata katika vyombo vya habari kwa matukio kama haya ambapo jamii ilichukulia hatua dhidi ya wahalifu waliokuwa wakishambulia wafanyabiashara wa Suneka na kisha kuachiliwa na polisi kwa kukosa ushahidi.