Habari za Kaunti

Peter Salasya asema anataka kuwa Gavana Kakamega 2027

January 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA LABAAN SHABAAN

MBUNGE wa Mumias Mashariki Peter Salasya ametangaza nia ya kuwania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Kakamega, uchaguzi mkuu ujao wa 2027.

Mtungasheria huyu mwenye utata alitumia mitandao ya kijamii kuweka paruwanja azma yake kumezea mate nafasi kubwa.

“Sasa ni wazi nitagombea Ugavana Kakamega,” Bw Salasya aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa X (awali Twitter) mnamo Jumapili Januari 21, 2024.

Gavana wa sasa Kakamega ni Bw Fernandes Barasa.

Mbunge huyu alitwaa kiti cha ubunge katika uchaguzi Mkuu wa 2022 kwa tikiti ya Democratic Action Party of Kenya (DAP-K).

DAP-K inaongozwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Bw Eugene Wamalwa ambaye pia ni mwanasiasa katika muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya.

Bw Salasya ni kiongozi mwenye uzushi na hutamba mitandaoni kwa utata wa mara kwa mara.

Soma pia https://taifaleo.nation.co.ke/makala/salasya-alaumu-shetani-kwa-kumpotosha

Si ajabu yamkini tangazo hili likachukuliwa kama njia mojawapo za kuchangamsha mitandao ya kijamii kwa njia ya kutafuta kiki.

Mnamo Januari 13, 2024, mbunge huyu anayehudumu muhula kwanza alikamatwa kwa madai ya kumshambulia diwani wa Malaha-Isongo-Makunga, Peter Indimuli walipohudhuria hafla ya mazishi Kaunti ya Kakamega.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inamtaka aandikishe taarifa kuhusiana na tukio hili.

Baada ya kutiwa nguvuni, mbunge Salasya aliachiliwa kwa bondi ya Sh50, 000.