Habari za Kaunti

Pigo Kaunti ikiagizwa kurejesha mapato yote iliyokusanya steji ya matatu tangu 2018

Na JOSEPH WANGUI October 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MVUTANO wa umiliki wa steji ya matatu kati ya Serikali ya Kitaifa na Kaunti ya Kiambu umechukua mwelekeo mpya baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Thika, kuamuru kaunti hiyo kurejesha mapato yote iliyokusanya kutoka kwa wahudumu wa matatu tangu mwaka wa 2018 hadi sasa.

Jaji Jacqueline Mogeni, aliamua kuwa Kaunti ya Kiambu inapaswa kulipa Shirika la Posta la Kenya (PCK), ambalo linadai kuwa ndilo mmiliki halali wa kipande cha ardhi kilichogeuzwa kuwa steji ya mabasi na serikali ya kaunti.

Mgogoro huo umekuwa ukishughulikiwa kwa zaidi ya miaka minane, ukihusu kipande cha ardhi kilichosajiliwa kama Kiambu/Municipality Block 2/284.

Shirika la Posta lilidai kuwa Kaunti ya Kiambu ilivamia ardhi hiyo kinyume cha sheria na kuanza kutoza ada kutoka kwa matatu bila idhini yoyote.

Mnamo Julai 13, 2018, Jaji Lucy Gacheru alitoa agizo la muda kuzuia kaunti kuendesha steji hiyo, kukata miti au kubomoa majengo, na kukusanya mapato kwenye eneo hilo.

Hata hivyo, Kaunti ya Kiambu ilidaiwa kupuuza maagizo hayo, na kuendelea na shughuli zake.

Mnamo Machi 2025, Shirika la Posta liliwasilisha ombi kaunti kuadhibiwa kwa kukaidi agizo la mahakama, likitaja Gavana Kimani Wamatangi na Karani wa Kaunti Peter Ndegwa.

Hata hivyo, Jaji Mogeni alikataa ombi hilo kwa kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja wa ukiukaji uliotajwa.

Licha ya hayo, mahakama ilikubali kuwa kaunti ilikiuka agizo la awali na ikasisitiza kwamba maagizo ya mahakama ni ya lazima na si hiari.

Hoja za mazungumzo kati ya pande husika hazikuweza kuhalalisha ukiukaji wa maagizo ya hivi punde.

“Mahakama haiwezi kutoa maagizo halafu yapuuzwe. Maagizo haya bado yapo na lazima yaheshimiwe,” alisema Jaji Mogeni.

Mahakama iliagiza kaunti ilipe PCK mapato yote yaliyokusanywa kwenye steji hiyo na maendeleo mengine yoyote kwenye ardhi hiyo tangu mwaka 2018.

Jaji Mogeni pia alikataa hoja ya kaunti kuwa kesi hiyo imepitwa na wakati, akieleza kuwa migogoro ya umiliki wa ardhi inadumu kwa muda wa hadi miaka 12.

Aidha, hoja ya kuwa suala hilo linapaswa kushughulikiwa kupitia mazungumzo ya kiutawala kwa mujibu wa Katiba (kifungu cha 189(3)) ilitupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi wa maelewano ya pamoja au mkataba rasmi.

Ripoti ya 2019 na madai ya mkutano wa Machi 2025 kati ya Kaunti na viongozi wa PCK hayakutambuliwa na mahakama kutokana na kukosekana kwa kumbukumbu rasmi.

Kwa mujibu wa maagizo mawili ya mahakama (ya 2018 na 2025), Kaunti ya Kiambu inapaswa kusitisha shughuli zote katika steji hiyo ya matatu na kurejesha mapato yote kwa Shirika la Posta.

Kukiuka maagizo hayo kunaweza kusababisha faini au kifungo kwa maafisa wa kaunti.

Wakati huo huo, kesi kuu ya umiliki wa ardhi bado inaendelea mahakamani.