Pigo kwa wafanyabiashara wa avokado usafirishaji baharini ukizimwa
WAFANYABIASHARA wa parachichi nchini wamepewa muda wa wiki moja kuondoa mzigo uliopo kabla ya serikali kufunga usafirishaji wa bidhaa hiyo kwa njia ya bahari kuanzia Oktoba 20.
Hatua hiyo inalenga kuzuia mauzo ya matunda ambayo hayajakomaa na kulinda sifa ya soko la Kenya nje ya nchi.
Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) ilisema Ijumaa kwamba mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa ni parachichi iliyokomaa ndio inasafirishwa nje ya nchi.
Mamlaka pia ilisema hatua hiyo itasaidia katika kulinda viwango vya mauzo ya nje, ambavyo vimekuwa vikichunguzwa na wanunuzi wa kimataifa katika miaka ya hivi majuzi kutokana na kuongezeka kwa usafirishaji wa parachichi ambayo haijakomaa.
‘Mamlaka imekuwa ikifuatilia mienendo hiyo na hivi majuzi ilifanya uchunguzi nchini kote katika kanda kuu za uzalishaji wa parachichi ili kubaini mwelekeo wa sasa wa uzalishaji na utabiri wa uzalishaji wa siku zijazo kwa msimu mkuu wa mwaka ujao,’ aliandika mkurugenzi mkuu wa AFA Dkt Bruno Linyiru katika notisi kwa wauzaji bidhaa hiyo nje.
‘Hakuna kibali kitakachotolewa kwa mafuta ya parachichi yaliyochakatwa nje ya nchi baada ya kufungwa kwa msimu wa kuvuna,’ lilisema shirika hilo, na kuongeza kuwa litapitia hali hiyo Januari mwaka ujao, kulingana na mwelekeo wa ukomavu na mifumo ya uzalishaji.