Habari za Kaunti

Polisi alivyomlipua mwanamume risasi kichwani katika purukushani ndani ya baa

Na GEORGE MUNENE November 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

AFISA wa polisi anayedaiwa alimuua mwanaume ndani ya baa katika soko la Ugweri Kaunti ya Embu wakati wakiburudika kwa pombe Jumatatu, alinyakwa na makachero.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Embu Samuel Muthamia alisema polisi huyo atashtakiwa kwa mauaji.

“Tulimkamata afisa huyo punde tu baada ya kutekeleza mauaji hayo. Suala hilo sasa linashughulikiwa kama la mauaji na afisa huyo atafikishwa kortini hivi karibuni,” akasema Bw Muthamia.

Kamanda huyo alisimulia jinsi alivyotembelea eneo la tukio na kuamrisha polisi huyo akamatwe.

“Kazi ya polisi ni kuwalinda raia na mali yao lakini si kuwaumiza. Tukio hili linasikitisha sana na halisawiri jukumu la polisi la kuwalinda raia kwa kuzingatia maadili ya kazi yao,” akasema Bw Muthamia.

Aliwataka wakazi na familia wasalie tulivu akiwahakikishia kuwa watatendewa haki.

Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, polisi wawili walivamia baa hiyo Jumamosi usiku na kusababisha waliokuwa wakiburudika kuchana mbuga ili kuzuia kukamatwa.

Ni wakati wa kutimkatimka huko ndipo walimwaangusha polisi mmoja naye aliposimama, alimmiminia mtu moja risasi na akafa papo hapo huku mwengine ambaye pia alilengwa na risasi akipata majeraha.

“Marehemu Ephantus Nyanga Muriithi, 43 ndiye aliaga kutokana na majeraha ya risasi kichwani huku mwenzake akijeruhiwa kwenye bega na bado amelazwa hospitalini. Ni kisa ambacho kimetuwacha tukiwa bado tumeshtuka,” akasema mkazi Kithaka Karukenya.

Familia ya marehemu ilisema kichwa chake kilipasuliwa na risasi na hakuna uwezekano wowote kuwa angenusurika.

“Mtoto wetu alikuwa ameketi wakati ambapo polisi hao walianzisha fujo na kuanza kufyatua risasi kiholela. Polisi ambaye alionekana kuwa alilewa pombe alianza kuwamiminia watu risasi,” akasema John Francis Nyaga ambaye ni mjomba wa marehemu.

Bw Nyaga, ambaye ni afisa wa ngazi ya juu ambaye amestaafu alisema kuwa hawatapumua hadi mshukiwa huyo ameadhibiwa na familia hiyo ikalipwa fidia kwa kumpoteza mwanao.

Wakazi walisema polisi waliwasili kwenye baa hiyo na kudai kuwa waliokuwa wakinywa pombe walikuwa wakiburudika nje ya muda uliowekwa. Wakazi hao pia sasa wanapanga kuandaa maandamano makubwa wakisaka haki.

“Tunataka haki na afisa aliyehusika lazima aadhibiwe vikali kisheria,”akasema Bi Gikeri.

Mwanaharakati wa Haki za Kibinadamu Taracisio Kawe alishutumu mauaji hayo na kusema uchunguzi wa ndani unastahili kufanyika na afisa huyo kushtakiwa kisha ahukumiwe vikali.

“Makachero wahakikishe hakuna cha mtu kukingwa kwa sababu familia hii sasa inaomboleza mwanao na wanastahili kupata haki,” akasema Bw Kawe.