• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:19 PM
Polisi amuua askari jela katika duka la pombe ya makali

Polisi amuua askari jela katika duka la pombe ya makali

NA EVANS JAOLA

HALI ya wasiwasi ilizuka mjini Kitale, Jumanne jioni, baada ya polisi wa utawala wa kiwango cha konstebo kumpiga risasi na kumuua askari jela katika duka la pombe ya makali almaarufu ‘wines and spirits’.

Kisa hicho kilifanyika karibu na Mahakama ya Kitale.

Haikubainika mara moja kuhusu sababu za polisi kumpiga risasi askari jela huyo.

Polisi walikuwa na kibarua kigumu kuudhibiti umati wa watu uliokimbia nyakati za jioni katika eneo la tukio kutazama kipi kilichokuwa kimejiri.

Polisi huyo pia alijipiga risasi na kujijeruhi vibaya kwenye jaribio la kujiua.

Kisa hicho kilifanyika mwendo wa saa kumi jioni.

Mshukiwa alimpiga risasi marehemu kwa kutumia bastola, baada ya wawili hao kugombana kuhusu suala ambalo halikubainika mara moja.

Baadhi ya wateja waliokuwa katika duka hilo, akiwemo askari jela mwingine, walitoroka baada ya kisa hicho.

Marehemu, ambaye ni dereva katika Gereza Kuu la Kitale, alikuwa akingoja kuwasafirisha mahabusu kutoka mahakama hiyo hadi kwenye gereza hilo.

Watu waliokuwa wakiendesha biashara zao katika eneo hilo walilazimka kuzifunga wakihofia usalama wao, baada ya polisi huyo kutishia kumdhuru mtu yeyote aliyekuwa karibu na eneo hilo.

Polisi walifanikiwa kumnyang’anya mshukiwa bastola hiyo na kumweka pingu, ambapo walimkimbiza katika Hospitali ya Kaunti ya Kitale ili kupata matibabu.

Kamishna wa Kaunti ya Trans Nzoia Gideon Oyagi, na Mkuu wa Polisi wa Trans Nzoia Magharibi Patrick Gaitariria walizuru eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Diwani aliyeuawa alikuwa msitari wa mbele kulaani ujangili

Wazazi sasa watoa watoto shule za kibinafsi kwa kulemewa na...

T L