Polisi matatani kwa dai la kuruhusu mshukiwa auawe
NA MWANGI MUIRURI
POLISI watano kutoka kituo cha polisi cha Murang’a huenda wakakamatwa na kushtakiwa kuhusiana na mauaji ya mhudumu wa bodaboda Jumapili iliyopita (Machi 24, 2024).
Inadaiwa maafisa hao wa usalama walipanga njama na kuchangia mauaji ya mhudumu huyo Brian Muchiri kwa tuhuma za kuwa mwizi wa simu.
Mmoja wa polisi hao aliweka picha ya Bw Muchiri akiwa ametiwa pingu mtandaoni na kuandika kuwa amemwonya mara kadha akomeshe wizi.
Pia, aliandika kuwa alale mahala pema kwenye jehanamu.
Kanda ya video ilionyesha polisi wakimsukuma Muchiri kwenye sehemu ya nyuma ya gari lao aina ya Landrover.
Baada ya hapo walianza kushauriana na wanafunzi wa chuoni waliokuwa wakimwandama mshukiwa badala ya kumtorosha.
Kisha, walimfungua pingu na kumsukuma nje ya gari na kuwaacha wanafunzi hao wampige hadi akafa huku nao wakienda na gari lao bila kuchukua hatua zozote.
Kamanda wa Polisi Murang’a, Bw Kainga Mathiu alisema suala hilo bado linachunguzwa na faili ya uchunguzi imefunguliwa.
“Uchunguzi unaendelea na matokeo yataonyesha jinsi mwanaume huyo alivyokufa na wale ambao walihusika na mauti yake, watachukuliwa hatua kali,” akasema Bw Mathiu.
Mratibu wa masuala, katika kamati ya wanabodaboda, Bw Stephen Mwangi, alidai kuwa afisa mmoja mwenye cheo cha juu aliwaagiza polisi hao wamwaache Muchiri mikononi mwa umma ili auawe.