Habari za Kaunti

Polisi Meru wanasa bunduki 4 kwa boma la mshukiwa

May 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI 

POLISI katika Kaunti ya Meru wamenasa bunduki nne, risasi 22, mapanga na sare za polisi kutoka kwa boma la mshukiwa mmoja wa ujambazi.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi ya kituo cha polisi cha Mutuati, mshukiwa hakukamatwa wakati wa operesheni hiyo kwa kuwa aliyelengwa alihepa baada ya kupata dokezi za kuviziwa.

Ripoti hiyo ilieleza kwamba maafisa hao walifika kwa boma la mshukiwa aliyetambuliwa kama Bw Ayub Kimathi katika kijiji cha Lodwar ambapo walipata silaha hizo.

“Nyumba yake ni ya vyumba vinne na ndani yake tulipata bunduki aina ya G3 ikiwa na risasi 22. Pia, kulikuwa na mapanga saba yaliyokuwa na makali ya kutisha, mkuki na pia sare za polisi,” ripoti hiyo ikasema.

Ripoti hiyo iliongeza kwamba polisi walipofanya msako zaidi katika uwanja wa boma hilo, walipata bunduki nyingine ya G3, ya AK-47 na bastola aina ya mini-beretta, zote zikiwa zimepakiwa kwa gunia na kufichwa vizuri.

“Lakini utaalamu wetu uliweza kutambua njama hiyo ya kuficha na tuliweza kutwaa shehena hiyo ya silaha na kuiwasilisha hadi kituo cha polisi ambapo sasa tunalenga kumnasa mshukiwa ndipo tumshtaki kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria,” ikasema ripoti hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilisema kuna uchunguzi zaidi ambao unaendelea kuwawezesha maafisa kubaini iwapo silaha hizo zishawahi kutumika katika visa vya uhalifu.

“Pia, tunataka kujua alizipata silaha hizo kwa njia ipi, mazingira gani na kwa lengo lipi,” ripoti hiyo ikaongezea.