• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Polisi wa akiba auawa na majangili Laikipia

Polisi wa akiba auawa na majangili Laikipia

NA MWANGI NDIRANGU

POLISI wa akiba (NPR) ameuawa kwa kupigwa risasi na wenzake watano kujeruhiwa na majangili waliotekeleza uvamizi katika kijiji cha Graton kilichoko Kaunti ya Laikipia.

Majangili walivamia boma la Bw Andrew Murugu mnamo Jumatatu usiku na kutoroka na ng’ombe 10 lakini wakafumaniwa na polisi wa akiba.

Kamishna wa Kaunti ya Laikipia Joseph Kanyiri alisema polisi hao wa akiba walikuwa wamefika kutibua wizi huo walipovamiwa na kundi jingine la majangili.

“Mifugo ilikuwa inasafirishwa kutoka maeneo ya bonde la Sieku ikielekezwa katika msitu wa Mukogodo na polisi wa akiba hawakujua kwamba kulikuwa na kundi jingine la majangili. Kulitokea ufyatulianaji mkali wa risasi wakati wa kujaribu kurejesha mifugo ambapo kwa bahati mbaya polisi mmoja alipoteza maisha,” akasema Bw Kanyiri.

Polisi wengine watano walipata majeraha ya risasi kwenye mikono na miguu lakini wanaendelea kupata nafuu katika hospitali ya Nanyuki Cottage.

Shambulio la hivi punde lilitokea katika eneo la Chumvi karibu na ranchi ya Borana ambapo vyombo vya usalama vimeonya kuna mtindo unaochipuka wa wezi wa mifugo kuilenga iliyoko kwenye ranchi za wamiliki binafsi.

Mapema Januari, iliripotiwa kwamba majangili waliokuwa wamejihami kwa silaha walisafirishwa kwa lori hadi katika ranchi ya Mugie kwenye barabara ya Rumuruti-Maralal na wakaiba ng’ombe 266 baada ya kuwalemea maafisa wa kutoa ulinzi hapo.

Wizi huo ulitokea siku nne tu baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kutembelea eneo hilo na kutangaza kujitolea kwa serikali kumaliza wizi wa mifugo katika eneo hilo.

Mifugo iliyoibwa kutoka kwa ranchi ya Mugie ilipelekwa hadi mjini Wamba na katika msitu wa Kirisia ulioko katika Kaunti ya Samburu. Maafisa kwa wiki tatu sasa, wamekuwa wakipekuwa kwenye maeneo hayo ambapo walifanikiwa kupata ng’ombe 100 pekee.

Viongozi wa kisiasa kutoka Kaunti ya Samburu wanalaumiwa kwa kutounga mkono juhudi za kusaka mifugo hata baada ya kupokea ng’ombe walioibwa na majangili wanaoshukiwa kutoka Kaunti ya Baringo kwenye hafla iliyoongozwa na Prof Kindiki.

“Mifugo iliyoibwa kutoka kwa ranchi ya Mugie mnamo Januari 2, 2023, imegawanywa makundi kisha kupelekwa kwa vijiji kadhaa katika Kaunti ya Samburu na tayari tumetambua pale ile inayokosekana iko. Lakini kwa bahati mbaya, hatuwezi tukaenda kuichukua kwa sababu ya changamoto za ardhi kimaumbile. Wito wetu ni kwa viongozi wa eneo hilo kuanzisha mazungumzo ya kutusaidia kurejesha mifugo,” akasema Bw Ivans Tomilson, mkurugenzi wa ranchi ya Mugie.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa wa mauaji ya Rita Waeni, raia wa Nigeria...

Seneta Wamatinga awataka viongozi Mlimani kudandia...

T L