Polisi waamriwa kuvunja Mungiki katika steji ya Sagana
NA MWANGI MUIRURI
KAMANDA wa polisi eneo la Kati, Lydia Ligami, ametoa amri kwa wadogo wake wanahudumu katika maeneo ya Kaunti ya Kirinyaga, wakabiliane na genge lenye sura ya Mungiki.
Bi Ligami alisema Jumatatu kwamba genge hilo linajaribu kudhibiti steji ya magari ya kutoka Sagana kuelekea Makutano, Thika, na Nairobi.
Kupitia ujumbe maalum kwa wakubwa wa polisi wa Kirinyaga, kamanda huyo alisema kundi hilo ni sharti lisakamwe.
“Tumepata ujumbe kutoka kwa wenyeji kwamba genge hilo linahangaisha wamiliki wa magari pamoja na abiria katika steji hiyo,” akasema Bi Ligami.
Alionya kwamba iwapo genge hilo litapewa nafasi ya kujiunda na kupata mizizi, litakuwa tishio kwa usalama.
“Genge hilo limejipa jukumu la kutoa idhini za uchukuzi na utumizi wa barabara za umma pamoja na kutoa ruhusa kwa abiria ili waendelee mbele na mipango yao ya kusafiri,” akasema.
Wamiliki wa matatu kutoka miji ya Nanyuki, Nyeri, Karatina, Embu, na Kagio walilalamika kwamba genge hilo limeyapiga marufuku magari ya aina hiyo kubebea katika steji hiyo ikiwa hawatakuwa wakilipa Sh200 kwa kila gari.
Madereva tulioongea nao walisema kwamba genge hilo liko na magari hata ya watu binafsi ambayo yamepewa ushirika wa kubeba katika steji hiyo.
“Hili genge linachuuza abiria na steji. Abiria wakiwa wengi, Kuna yale magari ambayo huitwa yabebe. Magari hayo huwa ni ya ushirika na genge hilo. Ukikaidi unapigwa na gari lako kuharibiwa,” akasema dereva mmoja.
Dereva mlalamishi aliongeza kwamba genge hilo hata linatekeleza utekaji nyara wa abiria na magari na kisha kuwaibia.