Polisi wamulikwa tena baada ya mwanamume kufa ndani ya seli saa chache baada ya kukamatwa
KWA mara nyingine, polisi wanamulikwa baada ya mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 26 aliyeripotiwa kupotea Nairobi wiki jana kupatikana mfu katika Kituo cha Polisi cha Central Mombasa saa kadhaa baada ya kukamatwa kwake.
Kulingana na ripoti za polisi, Simon Warui alikamatwa Septemba 17, 2025 katikati mwa jiji la Nairobi kwa tuhuma za wizi. Hii ni kufuatia malalamishi yaliyowasilishwa na mtu fulani.
Kutoweka kwake kulikuwa kumeripotiwa kutoka Mtaa wa Umoja, huku ripoti ikinakiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kamukunji.
Siku tatu baadaye, mkewe Warui alipokea simu kutoka kwa mlinzi wa kanisa lililoko kando ya barabara ya Nkurumah Mombasa, akimjulisha kwamba amezuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Central.
Mashahidi walisema Bw Warui alionekana mnyonge na mwenye msongo wa mawazo alipofikishwa katika kituo hicho.
Muda mfupi baadaye, aliomba atumie choo katika seli ambapo maafisa wa polisi waliripoti kuwa alianguka.
Walisema walisikia mlio mkubwa, na walipofanya ukaguzi, Warui alipatikana sakafuni damu ikimtoka kwenye pua.
Alikimbizwa katika hospitali moja ya karibu, lakini alikata roho pindi tu alipofikishwa katika kituo hicho cha afya.
Baadaye mwili wake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti kusubiri ufanyiwe upasuaji.
“Tuliambiwa kuwa alipatikana Mombasa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Central. Tuliwasili usiku na kushauriwa tusubiri hadi asubuhi. Tuliporejelea na kakake, tuliambiwa alikuwa amekufa.
“Hamna anayefahamu ikiwa alijiua au aliuawa. Tunataka Simon atendewe haki,” akasema binamu yake, Godfrey Gichuru.
Upasuaji uliofanyiwa maiti yake katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Coast General uligundua kuwa Bw Warui alikufa kutokana na jeraha shingoni lililosabishwa na kuanguka.