Polisi waokoa watoto 10 waliozuiliwa kanisani kwa ‘mafunzo ya utawa’
NA GITONGA MARETE
POLISI wa Timau, eneobunge la Buuri wanachunguza jinsi ambavyo kanisa moja limekuwa likiwazuilia wasichana wadogo kwa kisingizio cha kuwafunza kuwa watawa.
Watoto hao ni 10 na ni wa kati ya umri wa miaka minne na miaka 14.
Mnamo Jumatano, polisi walivamia Kanisa la Gospel of God International, Timau na kuwaokoa wasichana 10 waliokuwa wakizuiliwa katika chumba kimoja.
Kamanda wa Polisi wa Buuri Magharibi, James Musyimi alisema baada ya uchunguzi, wasichana hao walikuwa sawa ila walionekana kama watu waliokuwa wakipewa mafunzo yenye itikadi kali.
Bw Musyimi alisema walivamia kanisa hilo baada ya wahudumu wa afya wanaotoa chanjo kukatazwa kuwapa watoto chanjo kanisani humo.
Hata hivyo, mkuu huyo wa polisi alifichua kuwa, mchungaji John Maina ambaye ni mkuu wa kanisa hilo, bado hajakamatwa japo uchunguzi unaendelea.
“Bado tunamhoji pamoja na viongozi wengine wa kanisa. Tutakaporidhika kuwa kuna jambo kinyume cha sheria lililokuwa likiendelea, tutawakamata washukiwa na mkondo wa sheria utafuata,” akasema Bw Musyimi.
“Watoto hao wapo salama mikoni mwa polisi na tunashuku huenda haki zao zilikiukwa,” akaongeza.
Baadhi ya watoto wamekuwa kanisani humo tangu 2016.
Wakuu wa usalama akiwemo Mkuu wa Idara ya Upelelezi Meru, John Rioba mnamo Alhamisi walitembelea kanisa hilo na kuwahoji baadhi ya watu.
Makachero walisema huenda wasichana hao wamepokea mafunzo yenye itikadi kali kwa sababu hawaruhusiwi kupokea elimu ya shule za upili. Badala yake wamekuwa wakifundishwa ushonaji. Watoto hao walipelekewa hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kubaini iwapo walidhulumiwa kimapenzi.
Afisa mmoja wa idara ya watoto Timau alisema baadhi yao walikuwa wakitaka waungane tena na jamaa na familia zao.