• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Popo wafukuza wanajamii kutumia ukumbi wa Mkunumbi

Popo wafukuza wanajamii kutumia ukumbi wa Mkunumbi

NA KALUME KAZUNGU

UKUMBI wa kijamii wa Mkunumbi ulioko Lamu Magharibi ulipojengwa mwaka 2013, furaha ilisheheni miongoni mwa wakazi ambao matarajio yao yalikuwa ni ukumbi huo kuwabadilishia maisha.

Serikali ya Kaunti ya Lamu ndio iliyodhamini ujenzi wa ukumbi huo, ambapo mamilioni ya fedha za mlipa-ushuru yalitumika kuutengeneza.

Dhamira kuu ya jengo hilo ilikuwa ni litumiwe na wanajamii kuandaaa mikutano na hata sherehe mbalimbali za kijamii, zikiwemo za harusi.

Ukumbi huo una uwezo wa kutoshea zaidi ya watu 200 kwa wakati mmoja.

Cha kushangaza hata hivyo ni kuwa licha ya kuwepo kwa ukumbi huo, wananchi wamekuwa wakiukwepa, hivyo kuufanya kusalia mahame.

Je, ni nini kinachowasukuma wanajamii kuutoroka ukumbi huo?

Uchunguzi wa Taifa Jumapili umebaini kuwa popo waliokithiri ndani na nje ya ukumbi huo wa Mkunumbi ndio sababu kuu ya muundomsingi huo kutorokwa.

Ukumbi wa kijamii wa Mkunumbi, Lamu Magharibi. Popo wamevamia ukumbi huo na kusababisha wanajamii kuutoroka. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Maryam Ali, mkazi wa Mkunumbi, alikiri kuwa wanyama hao wamekuwa kero si haba kwani wamekuwa wakijitundika kwenye dari, kutani, madirishani na hata kwenye viti, hivyo kuyafanya mazingira ya ukumbi huo kuwa ya kuudhi.

Kulingana na Bi Ali, kinyesi cha popo kilichotapakaa kila mahali na hata manyoya ya wanyama hao, vimechangia harufu mbaya kusheheni ukumbini.

“Ni vigumu kwetu kuandaa mikutano au sherehe za aina yoyote kwenye ukumbi wetu. Popo ni wengi. Kila kukicha wanatapakaza kinyesi chao na kuchafua kuta na sakafu. Tumechoshwa nao. Wameacha ukumbi na uvundo ambao katu huwezi kuuvumilia. Ni kero, hivyo tumehama na kuwaachia hao popo huo ukumbi wautumie jinsi watakavyo,” akasema Bi Ali.

Naye Bw Yusuf Hassan, mkazi wa Mkunumbi, aliilaumu serikali ya Kaunti ya Lamu kwa kuutelekeza ukumbi huo punde ulipojengwa na kukamilika.

Bw Hassan anasema nyufa zimekithiri kila mahali kwenye ukumbi huo ilhali dari likivunjikavunjika, hivyo kuvutia popo hata zaidi kuishi kwenye jengo hilo lililotelekezwa.

Anasema kaunti haijakuwa ikifuatilia kwa karibu hali halisi ya ukumbi huo ambapo hata paa lake linavunja, hasa nyakati za mvua.

“Baada ya jengo kukamilishwa, serikali haijakuwa ikifuatilia ukumbi huu na kuuendeleza, ikiwemo kukarabati sehemu zenye nyufa. Na hii ndiyo sababu hawa popo wakapata mazingira ya kuishi wakijua fika jengo limetelekezwa. Kwa sasa paa linavuja. Dari limetobokatoboka na rangi kwenye kuta pia imechapa. Tumesalimu amri na kuachia jengo popo,” akasema Bw Hassan.

Wakazi hao waliiomba serikali ya kaunti ya Lamu kuzingatia kutekeleza ukarabati wa haraka wa ukumbi huo kwani kwa sasa jamii haina mahali maalumu kwa kuandalia makongamano na sherehe zao.

Sehemu ya dari lililovunjika, hivyo popo kujipatia makazi kwenye ukumbi wa kijamii wa Mkunumbi, Lamu Magharibi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Samson Kamau alisema kuwepo kwa popo kwenye ukumbi kumewawia vugumu wanajamii katika kutekeleza shughuli zozote ukumbini kwani wanyama hao pia wamekuwa wakipeperuka hewani kila wakati huku wakipiga kelele.

“Popo wa kujenga viota wamejenga. Wa kuchafua kuta na sakafu kwa mavi yao wamechafua. Kelele za kutisha zimesheheni pale ukumbini na ni vigumu hata kufanya mikutano au kufungisha watu nikaha kama ilivyokuwa ikifanyika awali. Tungeomba serikali yetu ya kaunti kukarabati ukumbi wetu. Pia wanunue viti vipya na sakafu ibadilishwe kwani hawa wanyama wameharibu kila kitu,” akasema Bw Kamau.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Vijana, Michezo na Jinsia katika Kaunti ya Lamu Sabastian Owanga, alisema tayari wametembelea ukumbi huo hivi majuzi na kwamba mipango inaendelea kuona kwamba ukarabati na utengenezaji wa jengo hilo unatekelezwa.

“Tunafahamu vyema hali ilivyo kwenye ukumbi wa Mkunumbi. Watu wasiwe na shaka. Mipango ipo ya kuukarabati na kuboresha miundomsingi pale. Watu wajue ukumbi huo utatengenezwa,” akasema Bw Owanga.

Waziri wa Elimu, Vijana, Michezo na Jinsia katika Kaunti ya Lamu Sabastian Owanga akihutubu. PICHA | KALUME KAZUNGU
  • Tags

You can share this post!

Diamond Platnumz aelekea ‘Zenji’ kumuomba Zuchu...

Shule yatoa hamasisho kuepusha watoto kuuawa mtaani

T L