Habari za Kaunti

Pwani ni salama kwa wote wanaotembea kwa likizo, polisi wasema

Na JURGEN NAMBEKA December 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

IDARA za usalama katika Kaunti ya Mombasa, zimewahakikishia Wakenya na watalii kutoka nje ya nchi usalama wao eneo hilo likitarajia wageni wengi wakati wa likizo za Krismasi.

Wakizungumza baada ya mkutano na washikadau kuzungumzia masuala mbalimbali ya usalama katika kaunti hiyo, walieleza kuwa polisi kutoka idara zote watahusika kuhakikisha kuwa msimu huo umekuwa wa amani.

Kamanda wa Polisi ukanda wa Pwani Bw George Seda, alisema tayari idara hiyo imewaweka polisi wa kutosha katika maeneo mbalimbali ambayo huenda yakakumbwa na changamoto wakati wa likizo hiyo.

Maeneo ya ufuoni

“Tumetuma polisi katika maeneo ya fuoni, kwenye barabara zinazoweza kushuhudia misongamano, na hata kwenye mahoteli ili tuwe na usalama saa 24,” akasema Bw Seda.

Kulingana naye, idara hiyo itakumbatia mfumo wa mashirika mbalimbali kuwajibikia usalama.“Nawahakikishia kuwa kila kitu ni sawa. Pwani ni salama, kuanzia hapa Mombasa, kuelekea Lamu , Kilifi na hata Kwale. Kujeni Pwani msherehekee hadi mtakapotaka kurejea nyumbani bila wasiwasi,” akasema kamanda huyo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Muungano wa washikadau wa Utalii eneo la Pwani (KCTA) Bw Victor Shitaka, tayari mikakati imewekwa, kuhakikisha wageni hawapati shida wanapozuru eneo hilo, ambalo hushusuhudia wageni wengi mwaka unapokaribia kukamilika.

SGR tayari imejaa

“Pwani ishaanza kupokea wageni. SGR tayari tumepata ripoti imejaa. Masuala yetu kuhusu usalama kwa watalii wa kigeni, wa humu nchini, na hata wafanyakazi katika sekta hiyo, tumeyazungumza na idara ya polisi. Tunataka kuwaambia Wakenya karibuni Pwani kwa sababu masuala ya usalama yameshughulikiwa,” akasema Bw Shitaka.

Kwa mujibu wa wadau, Pwani ilikuwa imejiandaa vilivyo ikiwemo kuwakaribisha wabunge kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambao kuanzia Desemba 3 hadi 18 watakuwa Pwani kwa michezo ya bunge ya ukanda huu.