Raia wa China aliyekuwa akisakwa Tanzania kwa mauaji akiri kumiliki bunduki Mombasa
RAIA wa China ambaye amekuwa akisakwa kwa madai ya mauaji Tanzania, amekiri mashtaka ya kumiliki bunduki na risasi kinyume cha sheria, na kupiga mtu Mombasa.
Ling Yao Zheng alidaiwa kutenda kosa hilo alipokuwa akijificha katika eneo la Likoni.
Mahakama ya Hakimu iliambiwa kuwa, mshukiwa alipatikana akiwa na bastola aina ya CZ P-10 C, iliyokuwa na risasi 13 bila kibali.
Katika shtaka la pili, Zheng alishtakiwa kwa kupiga na kusababisha madhara ya mwili. Mahakama iliambiwa alimpiga mwanamke aliyetambuliwa kama Jane Wambuga Mulei.
Upande wa mashtaka ulisema mshukiwa huyo alifanya makosa hayo mnamo Desemba 10, 2025, katika eneo la Shelly Beach, Likoni.
Kesi hiyo itatajwa tena Januari 19.
Taarifa zaonyesha kuwa, mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 42 anatafutwa na nchi jirani ya Tanzania kuhusiana na kisa cha kupiga risasi na kusababisha kifo kilichotokea Juni 11, 2022.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikimsaka Zheng kwa madai ya kumpiga risasi raia wa China mwenye umri wa miaka 26 katika orofa ya tatu ya jengo la makazi lililoko Barabara ya Kalenga, Ilala, Dar es Salaam.