Raia wa DRC anyimwa dhamana katika kesi ya Sh2.85bn
NA RICHARD MUNGUTI
RAIA wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeshtakiwa pamoja na Wakenya watano kwa kula njama ya kumlaghai mwekezaji kutoka Malaysia Dola 19 milioni (Sh2.85 bilioni) katika biashara ya kuuza dhahabu bandia, amenyimwa dhamana huku wenzake wakiachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni.
Bw Muke Wa Mansoni Didier (raia wa DRC) alielezwa na hakimu mwandamizi Bi Martha Nanzushi kwamba alitenda kosa hilo akiwa nje kwa dhamana katika kesi nyingine sawa na hiyo ya kufanya biashara ya kuuza dhahabu bandia.
Lakini Bi Nanzushi aliwaachilia Mabw Patrick Otieno Oduar, Brian Otieno Anyanga, Makfish Riogi Kabete, Ken Omondi Kimboi na Joshua Odhiambo Engade kwa dhamana ya Sh1 milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho ama walipe Sh500,000 pesa taslimu ndipo watoke.
Kesi hiyo imeorodheshwa kutajwa Januari 17, 2024, ndipo itengewe siku ya kusikilizwa.
Bw Didier alipelekwa kuzuiliwa katika gereza la Industrial Area.
Sita hao walishtakiwa kwa mara ya kwanza mnamo Desemba 28, 2023, mbele ya hakimu mwandamizi Bi Wandia Nyamu aliyeamuru wasalie gerezani hadi ombi lao la dhamana lisikilizwe na kuamuliwa.
Wote walikabiliwa na shtaka la kula njama kumlaghai Halid Bin Mohammed Yaacob Sh2.85 bilioni, wakidai walikuwa na kilo 500 za dhahabu ambayo wangemuuzia.
Washtakiwa hao pia walikabiliwa na shtaka la kujaribu kumwibia Bw Yaacob pesa hizo katika mtaa wa Kileleshwa jijini Nairobi.
Washtakiwa hao walitiwa nguvuni Desemba 27,2023, na maafisa wa polisi wa kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa raia wa Malaysia–Halid Bin Mohammed Yaacob–kwamba ameitishwa kiasi cha Dola 19 milioni (sawa na Sh2.85 bilioni) na washtakiwa hao wakidai wangemuuzia kilo 500 za dhahabu.
Upande wa mashtaka ulisema washtakiwa hao walianza njama hizo za kutaka kumlaghai Bw Yaacob kati ya Oktoba 19 na Desemba 27, 2023.
Mnamo Desemba 27, 2023, washtakiwa hao walijaribu kumwibia Bw Yaacob Sh2.85 bilioni kwa kumwonyesha vipande vya dhahabu bandia iliyokuwa imewekwa ndani ya masanduku.
Mahakama ilielezwa washtakiwa hao walijua wanamdanganya Bw Yaacob kwani hawakuwa na dhahabu hiyo.
Wakili Simon Mburu aliomba washtakiwa waachiliwe kwa dhamana lakini upande wa mashtaka ulipinga ombi hilo.
Mahakama iliamuru kesi hiyo itajwe mnamo Januari 17, 2024, kutengewa siku ya kusikilizwa.