Habari za Kaunti

Ruto akumbushwa atimize ahadi ya kutatua mizozo ya ardhi Pwani

Na VALENTINE OBARA September 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa eneo la Pwani wamemrai Rais William Ruto kutekeleza ahadi yake ya kutatua mizozo ya ardhi katika eneo hilo.

Suala la unyakuzi wa ardhi na uskwota lilikuwa mojawapo ya yale ambayo Rais Ruto aliahidi kutatua wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Mwaka uliopita, Rais Ruto aliwatwika jukumu Mawaziri Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Baharini), Salim Mvurya (Michezo) na Spika wa Seneti Amason Kingi, kutoa mwongozo wa ununuzi wa ardhi kutoka kwa mabwanyenye ili zigawanywe kwa maskwota.

Mapema mwaka huu, Rais alikariri tena mpango wa serikali ya kitaifa kununua ardhi ili zigawanywe kwa maskwota. Hata hivyo, hakujashuhudiwa hatua kubwa za kutekeleza mpango huo.

Wakizungumza jana katika uwanja wa Hospitali Kuu ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani, wanasiasa walisema ni muhimu tatizo hilo lisuluhishwe jinsi ilivyokuwa imepangwa.

“Shida kubwa hapa Pwani ni ya ardhi na maskwota. Tulikuja kwako Rais tukiwa na Joho, Mvurya na Kingi ukatuhakikishia utatafuta fedha, watatu hao wakae chini, wasuluhishe suala hilo. Bado tuna matumaini,” alisema Mbunge wa Kisauni, Bw Rashid Bedzimba.

Eneobunge la Kisauni ni mojawapo ya yale ambapo kuna idadi kubwa ya watu wanaoishi kama maskwota.

Hali hii husababisha mizozo ya mara kwa mara wakati watu wanapojitokeza kudai ndio wamiliki halali wa ardhi, na kusababisha nyumba kubomolewa na wakazi kufurushwa.

Msimamo sawa na huu ulitolewa na Seneta wa Mombasa, Bw Mohamed Faki, ambaye alipendekeza ushuru wa nyumba za bei nafuu utumiwe kununua ardhi kwa mabwanyenye na kugawia maskwota.

Vilevile, Bw Faki alipendekeza wananchi wawezeshwe kuomba fedha katika Hustler Fund kwa minajili ya kununua ardhi.

Akijibu suala hilo, Rais Ruto alitoa hakikisho kwamba mpango wa kununulia maskwota ardhi Pwani bado upo. Alisema tayari kuna mgao wa fedha kwenye bajeti ya mwaka huu, ambayo itatumiwa kutekeleza mpango huo.

“Kuhusu ardhi, tayari tuna mpango na bajeti katika mwaka huu wa kifedha. Hatimiliki 35,000 ziko tayari chini ya mpango huu na tutahakikisha tumetatua suala la ardhi jinsi tulivyoahidi,” akasema Dkt Ruto.

Wakati huo huo, Rais alipongeza utawala wa Kaunti ya Mombasa ukiongozwa na Gavana Abdulswamad Nassir kwa hatua zilizopigwa kuboresha huduma za afya.

Kulingana na Rais, ni kwa sababu ya uongozi bora ambapo Mombasa ilifanikiwa kuwa nafasi ya kwanza kwa usajiili wa watu katika Bima ya Afya ya Umma (SHIF), akisema asilimia 69 ya wakazi Mombasa wamesajiliwa katika hazina hiyo ya kitaifa.

Bw Nassir alisema uongozi wake utazidi kuwekeza katika uboreshaji wa huduma za afya kwa kujenga miundomsingi zaidi na kutoa mazingara bora kwa wahudumu wa afya.