Ruto amkwamilia Raila kwa kutekeleza matakwa yake
Katika kile kinachoonekana kama hatua ya kisiasa ya kumbembeleza kiongozi wa ODM Raila Odinga kuelekea 2027, Rais William Ruto ametangaza mpango wa kuwalipa fidia wahanga wa machafuko yaliyotokea wakati wa maandamano dhidi ya serikali tangu mwaka wa 2017.
Kupitia taarifa aliyotoa Ijumaa, Agosti 8, 2025, Dkt Ruto alisema serikali yake itafidia familia za raia waliopoteza maisha na maafisa wa usalama waliojeruhiwa au kufa wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na polisi.
“Hatua hii imejikita katika hitaji la Katiba la kuhakikisha uwajibikaji na utekelezaji wa haki na uhuru wa raia,” alisema Rais Ruto, akisisitiza kuwa ni muhimu kutambua mateso ya wahanga wote wa maandamano wawe raia na maafisa wa usalama.
Mpango huo maalum wa siku 120 utaongozwa na Mshauri wa Rais kuhusu Haki za Kibinadamu, Prof Makau Mutua, kwa ushirikiano na ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Usalama, Fedha, na taasisi nyingine husika.
Hatua hii imejiri baada ya shinikizo kali kutoka kwa chama cha ODM na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, wakitaka serikali iwajibike kwa vifo na majeraha yaliyotokea hasa wakati wa maandamano ya 2024 na 2025.
ODM imeunda kamati ya ndani ya kuchunguza utekelezaji wa mkataba wake na UDA, huku ikisemekana viongozi wakuu wamegawanyika.
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna amekuwa akilalamikia serikali kwa kukaidi mkataba wa ushirikiano baina ya UDA na ODM kwa kutolipa fidia hadi sasa.
Huku akipinga ODM kumuunga mkono Ruto 2027, Bw Sifuna amedai kwamba okitokea hali hiyo, atajiuzulu na kujiunga na vuguvugu jipya la Kenya Moja linakalopinga juhudi zozote za Rais kuwania muhula wa pili.
Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNHCR), zaidi ya watu 159 wameuawa na polisi wakati wa maandamano tangu Juni 2024.
Mbali na mpango wa fidia, Ruto na Raila pia wametangaza kuundwa kwa kamati ya kiufundi ya wanachama watano kusimamia utekelezaji wa mapendekezo 10 ya ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO). Kamati hiyo itaongozwa na Agnes Zani na kujumuisha wanasiasa na wanaharakati wa pande zote mbili.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuanzishwa kwa Ofisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani, Ofisi ya Waziri Mkuu, na mageuzi ya mfumo wa uchaguzi. Ingawa baadhi ya mapendekezo yamecheleweshwa, Rais Ruto ameahidi kuyatekeleza kikamilifu, pamoja na kulinda haki ya maandamano ya amani.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Raila alisema japo hana nia ya kujiondoa mapema kutoka kwa serikali ya ushirikiano iliyoanzishwa mwaka jana, atakuwa upande wa Ruto hadi 2027. “Tumesema tupo ndani ya serikali hadi 2027. Baada ya hapo, ni suala litakaloamuliwa na wanachama wa chama, si Raila Odinga peke yake,” alisema.
Kuhusu tetesi za kuungwa mkono na Raila kwa muhula wa pili, Ruto hajaweka wazi nia hiyo, lakini wandani wake ndani ya ODM tayari wameashiria uwezekano wa kutangaza “Ruto-Tosha.”
Mbunge wa Alego Usonga, Sam Atandi, alisema: “Tuna deni kwa Ruto. Alisimama na Raila mwaka 2007. Ni wakati wetu kumrudishia mkono.” Mbunge wa Uriri, Mark Nyamita, aliongeza: “Hatujawahi kuona rais ambaye ametujali kama Ruto. Hakuna atakayetufanya tubadilishe nia.”
Hali hii inatoa taswira ya mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini, huku Rais Ruto akizidi kuchukua hatua zinazodhihirisha ushirikiano wa karibu na Bw Odinga – hatua ambazo kwa wengi ni ishara tosha kuwa Ruto sasa anamkumbatia Raila, kisiasa na kimaamuzi.