Sababu za Gavana Sang kubadili sura ya baraza la mawaziri Nandi
GAVANA wa Nandi Stephen Sang amefanya mabadiliko katika baraza la mawaziri wa kaunti hiyo.
Wakati huo huo, Bw Sang alithibitisha kujiuzulu kwa kwa mawaziri wawili – Ruth Koech (Afya) na Drice Rono (Uchukuzi).
Akitangaza mabadiliko hayo, Gavana Sang alimpa Dkt Yulita Mitei wizara ya Afya na Usafi kuwa Kaimu Waziri.
Mkuu huyu wa kaunti aliwasilisha majina ya mawaziri watatu kwa bunge la kaunti kutaka waidhinishwe.
Bw Sang aliwateua Dkt Viola Chemogos (Afya), Bi Reney Kirwa (Elimu) na Bw Robert Limo (Uchukuzi) akipigia debe hatua hii itaboresha utoaji huduma.
Akizungumza katika makao makuu ya kaunti, gavana aliwapa baadhi ya mawaziri majukumu mapya.
Bw Alfred Lagat akitwikwa wadhifa wa wizara ya Ardhi, Mazingira, na Mabadiliko ya Tabianchi.
Dkt Philemon Bureti alikabidhiwa Wizara ya Biashara na Utalii huku Bw Isaiah Keter akisalia na Wizara ya Utawala, Utumishi wa Umma na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na kuwa Kaimu Waziri wa Michezo, Sanaa na Masuala ya Vijana.
Gavana Sang anakaribia kumaliza muhula wake wa pili kuongoza kaunti hiyo ya bonde la ufa.
Isitoshe Bw Sang alifanya mabadiliko kwa nyadhifa za makatibu wa kaunti.
Bi Beatrice Chemurgor (Elimu), Bw Benjamin Kiprotich (Utamaduni na Maslahi ya Jamii), Caroline Lagat (Biashara na Utalii), Bw Joseph Cheruiyot (Michezo na Masuala ya Vijana) na Dkt Paul Sang’a (Kilimo na Ustawishaji wa Vyama vya Ushirika).
Walioteuliwa watapigwa msasa na bunge la kaunti.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan