• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Sakaja awasilisha mswada wa kuongeza urefu wa majumba

Sakaja awasilisha mswada wa kuongeza urefu wa majumba

NA NDUBI MOTURI

GAVANA Johnson Sakaja (pichani) amechukua hatua za kurasimisha pendekezo lake la kuondoa hitaji la kikoloni, kwamba majumba jijini Nairobi yasizidi orofa 15.

Bw Sakaja anataka urefu wa majumba katikati mwa jiji kuu uongezwe hadi orofa 75.

Katika mitaa ya kifahari kama vile Kilimani, Kileleshwa na Muthangari majengo yataruhusiwa kuzidi orofa 15.

Maeneo yaliyo kando ya barabara ya Ngong yatakuwa na majumba yasiyozidi orofa 25 huku Lower Spring Valley — inayojumuisha Mathare River, barabara ya Westlands Redhill Link, Waiyaki Way na Ring Road Parklands — yakiwa na majumba ya orofa nne, iwapo pendekezo la Sakaja katika mswada mpya litapitishwa na bunge la kaunti.

Tayari, mswada umewasilishwa kwa Kamati ya Bunge la Kaunti ya Nairobi kuhusu Mipango inayoongozwa na diwani wa Kitisuru, Alvin Palapala.

Hili ni jaribio la pili la serikali ya kaunti kurekebisha kanuni za ujenzi wa majumba, ambazo hazibadilishwa tangu 2004.

Jaribio la kwanza lilifanywa na iliyokuwa Shirika la Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) ila liligonga mwamba baada ya muhula wa shirika hilo kutamatika kabla sera husika kupitishwa na bunge la kaunti.

Maeneo kama Westlands, katikati mwa jiji, Museum Hill na viunga vyake yamewekwa katika zoni ya tatu ambayo majumba hayafai kuzidi orofa 30.

Bw Palapala aliambia Taifa Leo kwamba bunge la kaunti litaunga mkono mapendekezo hayo mapya kwa sharti kwamba serikali ya kaunti itaweka mfumo unaofaa wa miundo msingi ili kutimiza mahitaji ya wakazi maradufu watakaofurika jijini kutokana na ongezeko la vyumba zaidi .

“Hatupingi pendekezo hili ikizingatiwa kuwa mipangilio ya ujenzi imevurugika katika kaunti hii. Kama kamati, tulikutana na serikali ya kaunti tukafanya majadiliano. Msimamo wetu uko wazi kwamba ni lazima kuwe na maji safi ysa kutosha, barabara zipanuliwe na mabomba ya kuondoa majitaka yaongezwe ili kufanikisha ongezeko hilo la vyumba zaidi,” alisema.

Diwani huyo alisema mabadiliko hayo pia yatahitaji kundi la watalaamu ambao watatathmini kwa kina mfumokazi uliopendekezwa na kuandaa wa uhalisia kwa kuzingatia mahitaji ya wakazi.

“Tumependekeza kundi la wataalamu kutoka bunge la kaunti na serikali ya kaunti kuchambua mfumokazi. Tutazingatia ushauri wao kabla kupitisha pendekezo,” aliohoji.

Katika sera hiyo mpya, maeneo ya katikati mwa jiji zikiwemo barabara za Uhuru Highway, Tom Mboya, Haile Selassie na University Way yamewekwa katika zoni ya kwanza ambayo majumba yatakuwa na orofa 75. Katika jiji jipya la Railways City majumba hayatazidi orofa 50.

Maeneo yaliyo kwenye barabara za Valley Road, Dennis Pritt, Ralph Bunche na State House yataruhusiwa kuwa na majumba yenye orofa 25 sawa na maeneo yaliyo kwenye barabara za Argwings Kodhek , Ngong, Hospital, Upperhill Link na Mbagathi Way.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke aliyeangamia Shakahola na mtoto alitafuta mhubiri...

Pombe: Hoteli 5 zafungwa msako ukiendelea

T L