Seneta alalamikia unyakuzi wa ardhi Mombasa
NA WINNIE ATIENO
SENETA wa Mombasa Bw Mohammed Faki amesihi viongozi wa kaunti hiyo kushirikiana ili kurejesha vipande vya ardhi vilivyonyakuliwa na mabwanyenye.
Akiongea eneo la Likoni kwenye mchuano wa kandanda miongoni mwa vijana, Bw Faki alilalamikia ardhi nyingi kunyakuliwa na mabwanyenye.
“Kuna viwanja vingi ambavyo vimenyakuliwa na mabwanyenye, kwa mfano; Caltex imeshanyakuliwa. Huo uwanaja tulikuwa tunautumia kwenye mikutano ya kisiasa. Huo uwanja ni wa jamii,” akadai Bw Faki.
Alisema waumini wa dini ya Kiislamu pia wamekuwa wakitumia uwanja huo kuswali.
“Yule ambaye anadai umiliki awachane na kiwanja hicho. Tutahakikisha tunachukua kiwanja hicho,” akasisitiza.
Alisihi wawakilishi wa wadi eneobunge la Likoni kulinda viwanja vya umma dhidi ya wanyakuzi.
Vile vile alimsihi Gavana Abdulswamad Nassir (Mombasa) kukarabati viwanja vya michezo ili vijana wavitumie kukuza talanta zao.
“Viwanja vingi vina mabonde, tunamsihi Gavana Nassir azikarabati,” alisema Bw Faki.
Kaunti hiyo imekumbwa na unyakuzi mkubwa wa ardhi huku wanasiasa wakilaumu baadhi ya viongozi wa Mombasa kwa unyakuzi huo.