Seneta: Mishahara yalemaza maendeleo Taita Taveta
NA LUCY MKANYIKA
SENETA wa Kaunti ya Taita Taveta Jones Mwaruma amelalamika kuwa mzigo mkubwa wa mishahara ya wafanyakazi wa kaunti hiyo unaathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika serikali hiyo.
Akihutubia bunge la kaunti hiyo mjini Wundanyi, seneta huyo alitoa wito kwa Gavana Andrew Mwadime kupunguza kuajiri wafanyakazi wapya ili kupunguza mzigo wa mishahara ambao unachukua asilimia 56 ya bajeti ya serikali hiyo.
Kwa sasa, serikali hiyo hutumia takriban Sh3.5 bilioni kulipia mishahara ya wafanyakazi wake dhidi ya Sh5.2 bilioni za mgao kutoka kwa serikali kuu. Kulingana na sheria mishahara haipaswi kupita asilimia 35 ya mgao wa kaunti.
Seneta Mwaruma alisema kuwa hatua hii ni muhimu ili kuelekeza fedha zaidi katika miradi ya maendeleo ambayo itawanufaisha wananchi moja kwa moja.
“Kila uchao serikali ya kaunti inatoa matangazo ya kuajiri wafanyakazi. Hili ni swala ambalo linahitaji kufikiriwa kwani tutapata wapi pesa za maendeleo,” alisema Bw Mwaruma.
Huku suala la kupunguza wafanyakazi likihitaji utaratibu maalum na uangalifu ili kuepuka kuvuruga huduma za kaunti, seneta Mwaruma alipendekeza kuwa wafanyakazi wa sekta muhimu pekee kuajiriwa.
“Tukiendelea hivi hatutapata pesa za kutekeleza miradi ya maendeleo. Ikiwa ni lazima wafanyakazi waajariwe basi iwe ni katika idara muhimu pekee ili kutopunguza ufanisi katika utoaji wa huduma za kaunti,” alisema.
Hotuba ya seneta Mwaruma inajiri baada ya wawakilishi bunge la kaunti hiyo kumshambulia wiki jana baada ya seneta huyo kushtumu wawakilishi wadi kwa kuvunjilia mbali hazina ya mkopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
Wakiongozwa na naibu spika Bw Anselm Mwadime, wawakilishi hao walimtaka seneta Mwaruma kufika bungeni ili kueleza kuhusu maswala ambayo alihisi yanaenda mrama.
“Uongozi ni kuongozana, kila siku unatushambulia kwa mitandao na hujawahi kutuita tushauriane kuhusu maswala yanayokabili kaunti hii. Hatutakubali maana sote tulichaguliwa na wananchi. Ukituhitaji uje bungeni tushauriane mambo ya kaunti yetu,” alisema.
Hata hivyo, mnamo Jumanne baadhi ya wawakilishi wadi walikosa kuhudhuria kikao hicho cha hutuba ya seneta Mwaruma.
Vilevile, wale waliohudhuria walionekana kutoshabikia hotuba yake.
Katika hotuba yake, Bw Mwaruma aliwataka wawakilishi hao kurudisha hazina hiyo ya mkopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kuhakikisha kuwa fedha za umma zinalindwa, na vilevile kuna uwajibikaji katika serikali ya Gavana Mwadime.
“Ni muhimu kuangalia yale malengo ambayo serikali ya kaunti imefikia ili kujua ni lipi linahitaji kushughulikiwa,” akasema.